Na Eva Godwin-DODOMA
SERIKALI kupitia Mtakwimu Mkuu wa Dkt. Albina Chuwa inaendelea kutoa fedha za kutosha kutekeleza zoezi la Sensa kwa kutoa mafunzo kwa Makarani na Wasimamizi wa Sensa 205,000 ambayo ni mafunzo ngazi ya tatu na ya mwisho kabla ya kufanyika kwa zoezi la kuhesabu Watu.
Ameyazungumza hayo leo 11 Agosti, 2022 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Takwimu Jijini Dodoma.
Amesema hadi kufikia tarehe 05 Agosti 2022 Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar zimeshatuma fedha za Mafunzo ya siku 16 kwa Makarani wa Kawaida na siku 15 kwa Makarani waandamizi, Wasimamizi wa Maudhui na Wasimamizi wa TEHAMA.
“Fedha hizi zimetumwa kwenye Akaunti za Hazina ndogo za kila Mkoa na Mchakato wa malipo unafanyika kwa mujibu wa taratibu za Serikali, na kwenye mafunzo haya ya Sensa ngazi ya Wilaya kuna washiriki wa makundi ya aina kuu mawili”, amesema
“Kundi la kwanza ni wakufunzi ambao sio watumishi wa Serikali na pia Kundi la pili ni Makarani na Wasimamizi wa Sensa bila kujali kama ni watumishi wa Serikali au sio Watumishi wa Serikali”.Amesema Chuwa
Aidha amesema ili kudhibiti ubora wa mafunzo hayo Menejimenti ya ofisi ya Taifa ya Takwimu, Viongozi wengine wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali wamefanya ziara katika vituo vya Mafunzo na wamebaini kuwa baadhi ya vituo vya mafunzo vinahitaji kuongezewa nguvu kwa kuongezewa wakufunzi.
“Watumishi wa Serikali katika kutekeleza Majukumu yao watalazimika kutembelea vituo vya mafunzo ndani ya Mkoa husika kwa lengo la kuhakikisha kila kituo kina idadi sahihi ya Walimu kulingana na Mahitaji”, amesema
“Kutokana na Majukumu hayo, Wakufunzi wote ambao ni Watumishi wa Umma watakipwa kwa utaratibu ambao umehusishwa na utatumwa tena kwao kupitia waratibu wa Sensa wa Mikoa na Wilaya kesho tarehe 12 Agosti, 2022”. Amesema
Ameongezea kwa kusema kuwa Fedha zinazotumika kwenye zoezi hili ni za Serikali na Malipo ya Maafisa wanaoshiriki kwenye zoezi hili ni lazima yaendane na miongozo ya Serikali.
“Watumishi wa Serikali wanadhima ya kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa na hivyo ushiriki wao ni kutokana na nafasi waliyo nayo kama Watumishi Serikalini
“Naomba kuwafahamisha kwamba mafanikio ya zoezi hili kwenye eneo lako na kipimo cha utumishi wako na uzalendo wa Nchi yako, na hili kuharakisha malipo ya washiriki wa mafunzo haya nawaagiza waratibu wa Sensa wote ngazi ya Mkoa na Wilaya kuharakisha mchakato wa malipo ndani ya Muda, na malipo hayo yafanyike kwa kufuata taratibu za Serikali na niwaombe Watendaji, Wakurugenzi wayendaji wa Halmashauri zote Nchini kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Waratibu wao kuhusu malipo”. Amesema Chuwa