Featured Kitaifa

BENKI YA USHIRIKA MBIONI KUANZISHWA

Written by mzalendoeditor

 

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 9,2022 wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Sekta ya ushirika kwa mwaka 2021/2022 na Mpango wa Kuimarisha Ushirika kwa Mwaka 2022/2023.Kushoto kwa Mrajis ni Naibu Mrajis,Bi. Consolatha Kiluma.

 

………………………………………

Na Alex Sonna-MBEYA

KATIKA  Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imepanga kutekeleza mambo tisa ikiwemo kuratibu uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ili kuchochea maendeleo ya Ushirika nchini.

Hayo yameelezwa leo Agosti 9,2022 Jijini Mbeya na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo,Dk Benson Ndiege wakati akieleza mwelekeo wa bajeti ya tume hiyo kwa mwaka 2022-2023.

Mkurugenzi huyo amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ushirika unahamasishwa miongoni mwa watanzania kiuchumi na kusimamiwa kwa mujibu sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha waanushirika.

Amesema kwa mwaka 2022-2023 wamepanga kufanya uthamini wa mali zinazomilikiwa na vyama  vya Ushirika kwa lengo la kutambua thamani halisi ya soko ya mali hizo na hivyo kuviwezesha vyama kufanya uwekezaji wenye tija.

Pia,kuanzisha Mfuko wa Bima ya Akiba na Amana za SACCOS utakaotumika kama kinga ya akiba na amana za wanachama wa SACCOS ambao SACCOS zao zitashindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria;

Vilevile,kuimarisha udhibiti na usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa kutoa mafunzo kwa maafisa Ushirika 226, Kukagua vyama vyote, na kuendelea kununua vitendea kazi na kununua magari  kwa ajili ya kuongeza tija kwa maafisa ushirika. Katika mwaka husika manne (6) na pikipiki 50 na komputa 200 zitanunuliwa;

“Kuanza matumizi ya mfumo wa usimamizi na ukaguzi wa vyama vya ushirika na kuhamasisha, kuratibu na kusimamia ujenzi na ufufuaji wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao. 

“Kwa mfano, Tume inasimamia ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho cha TANECU, Tume inaratibu ujenzi wa viwanda vya wanawake kupitia chama cha ushirika wa wanawake cha Madirisha,”amesema Mkurugenzi.

Vilevile,kuratibu na hamasisha ujenzi wa maghala ya mazao ya kilimo ili kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha mfumo wa minada ya mazao yanayozalishwa na wananchi;

Pia,kutengeneza utaratibu wa uwezeshwaji vyama vya ushirika (cooperative facilitation scheme) ili kuongeza ufanisi wa vyama vya ushirika; na

“Tume itaimarisha zaidi matumizi ya Vyombo vya Habari (TV, Redio na Mitandao ya Kijamii) katika uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika na manufaa ya kuwa katika Ushirika,”amesema Mkurugenzi huyo.

UTEKELEZAJI KATIKA MWAKA 2021/ 2022

Amesema dhamira ya Serikali ni kutumia mfumo wa ushirika katika kuwewezesha wananchi kiuchumi na kuchangia ipasavyo katika ustawi wao na wa Taifa kwa ujumla.

”Katika kutekeleza hili, kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha Ushirika unahamasishwa miongoni wa watanzania na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha wanaushirika,”amesema

VIPAUMBELE

Katika kutekeleza dhamira hiyo, tume katika mwaka 2021/2022, ilijiwekea vipaumbele vya utekelezaji hususan katika maeneo ya kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika.

Pia,kuratibu uhamasishaji, utafiti na utoaji wa elimu ya maendeleo ya Ushirika na kuimarisha masoko, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

UHAMASISHAJI WA UANZISHWAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA

Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, idadi ya Vyama vilivyosajiliwa ilifikia 9,741 ikilinganishwa na Vyama 9,185 katika kipindi hicho cha mwaka 2021.

Kati ya vyama vilivyosajiliwa, 4,538 ni vyama vya ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS), 3,946 ni Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na 1,257 ni Vyama vinavyojishughulisha na kazi mbalimbali zikiwemo ufugaji nyuki, ufugaji, madini na uvuvi.

Aidha, idadi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka wanachama 6,050,324 mwaka 2020/2021 kufikia wanachama 6,965,272 kwa mwaka 2021/2022.

“Uhamasishaji umejielekeza Zaidi kwenye mazao au aeneo ambayo ambayo huko nyuma hayakupewa kipaumbele au hayakuudumiwa na ushirika,”amesema Mkurugenzi huyo.

UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA

Mkurugenzi huyo amesema tume katika mwaka 2021/2022, iliendelea kuimarisha ukaguzi katika Vyama vya Ushirika, ambapo kati ya Julai 2021 na Juni 2022, Vyama vya Ushirika 6,013 kati ya Vyama 9,185 vilikaguliwa.

Amesema matokeo ya ukaguzi huo ni pamoja na kubainika kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa Vyama vya Ushirika, na hivyo kusababisha kutokea kwa upotevu au hasara ya fedha na mali kwa baadhi ya Vyama vya Ushirika.

Aidha, imebainika kuwa Vyama vya Ushirika vina mifumo mibovu ya udhibiti wa ndani.  

Pia, baadhi ya vyama vinashindwa kuandika miamala ya fedha kulingana na taratibu za fedha zilizopo.

Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwatengua viongozi 17 wa Bodi za Vyama viwili (2) vya Upili na wajumbe 224 wa Bodi katika Vyama vya Msingi 32 kutoka Mikoa 15 walioshindwa kusimamia vyama vyao ipasavyo.

Aidha,viongozi waliobainika kuhusika na vitendo vya wizi na ubadhirifu wamefikishwa kwenye vyombo vya Dola kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.

“Kesi 23 (madai 21 na jinai 2) zimefuguliwa kuhusu Mashauri mbalimbali ya Vyama vya Ushirika katika Mahakama kote nchini,”amesema Dk Ndiege.

Pia tume imeendelea kushirikiana na wadau kama kutoa elimu kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika.  

KUIMARISHA USIMAMIZI WA VYAMA VYA USHIRIKA

Katika Kuimarisha usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini, Tume imetekleza kuwajengea uwezo Maafisa Ushirika nchini na viongozi wa vyama vya ushirika.

Amesema ili kukabiliana na changamoto ya utendaji usioridhisha na ubadhirifu katika Vyama vya Ushirika, Tume kati ya Julai 2021 na Juni 2022 imewajengea uwezo maafisa ushirika 170 kutoka mikoa 13.

Mikoa hiyo ni  Mwanza, Tabora, Shinyanga, Geita, Mara, Kigoma, Kagera, Simiyu, Iringa, Njombe, Mtwara, Ruvuma na Lindi.

Aidha, viongozi 17,423 na wanachama 197,968 wa vyama vya ushirika walipatiwa mafunzo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa vyama.

UNUNUZI WA VITENDEA KAZI

Katika kuimarisha utendaji kazi wa maafisa Ushirika nchini, tume ilinunua vitendea kazi ambavyo ni magari 12, pikipiki 137 na Kompyuta 82.

Amesema vitendea kazi hivi vimegawanywa kwa Maafisa Ushirika kote nchini.

UANDAAJI WA MIONGOZO MBALIMBALI

Katika kuimarisha Usimamizi wa Vyama vya Ushirika, tume katika mwaka wa fedha 2021/2022 imeandaa miongozo 15 itakayotumika katika kusimamia Vyama vya Ushirika nchini.

Amesema miongozo hiyo inahusu maeneo ya ufilisi, uwekezaji na usajili wa rehani, utatuzi wa migogoro, ukaguzi wa vyama  vya Ushirika visivyo vya kifedha.

Pia, ukaguzi wa Vyama vya Ushirika vya kifedha, udhibiti wa majanga, uwekezaji, mawasiliano, utumishi, ununuzi kwenye Vyama vya Ushirika, uanzishaji na uendeshaji wa mifuko ya pembejeo na usimamizi wa AMCOS za miwa nchini.

USIMAMIZI WA VYAMA VYA USHIRKA WA KIFEDHA

Dk Ndiege amesema tume imeendelea kutoa leseni za uendeshaji wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo kwa mujibu wa Sheia ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.

Amesema Katika mwaka 2021/2022 SACCOS 258 zimepatiwa Leseni na hivyo kufanya idadi ya SACCOS zenye leseni kufikia 691.

Amesema kati ya hizo, SACCOS daraja A ni 559 na SACCOS daraja B ni 132.

Adha, hadi kufikia Juni 2022, SACCOS zilizopatiwa leseni zilikuwa na hisa ya zaidi ya Sh bilioni  134, mali zaidi ya  Shilingi bilioni 836 Akiba na amana ni zaidi ya  Shilingi bilioni  576 na mikopo iliyotolewa kwa wanachama ni zaidi ya shilingi bilioni  639.

KUIMARISHA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO KUPITIA USHIRIKA

Amesema manufaa ya Ushirika ni pamoja na urahisi wa upatikanaji wa pembejeo kwa Vyama vya Ushirika wa mazao.

KUIMARISHA MASOKO YA MAZAO NA BIDHAA ZA USHIRIKA

Katika kipindi cha mwaka husika, tume ililenga kuimarisha masoko kwa mazao na bidhaa za Ushirika ambapo iliingia Makubaliano (MoU) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ya kuboresha miundombinu ya ufanyaji biashara.

Aidha, Tume ya Maendeleo ya Ushirika imetoa mafunzo ya biashara na masoko kwa watendaji na viongozi wakuu wa Vyama Vikuu vya Ushirika 156 ili kuwawezesha kutafuta masoko ya mazao yao ndani nan je ya nchi.

KUHAMASISHA WANAWAKE KUJIUNGA NA USHIRIKA

Amesema tume imeendelea kuhamasisha Wanawake ambao, Wajasiriamali, Wafanyabiashara, Wafugaji, Wavuvi, Wasusi, Mafundi, Wakulima na wazalishaji kwenye shughuli nyingine za kiuchumi za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu au mahitaji maalum kujiunga pamoja na kuanzisha Ushirika utakaokuwa “Multipurpose” kwa kutumia muundo wa Madirisha “Business Model”.

“Hii ni utekelezaji wa Mikataba na Maazimio mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025,”amesema

KUIMARISHA MITAJI NA UWEKEZAJI KATIKA VYAMA VYA USHIRIKA

Tume ya Maendeleo ya Ushirika imehamasisha na kuwezesha Vyama vya Ushirika kufufua na kuanzisha viwanda ili kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa katika vyama hivyo.

Amesema Viwanda vinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka 374 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 452 mwaka 2021/2022.

Aidha, Tume imeendelea kuhamasisha Vyama Vikuu vya Ushirika kuanzisha kampuni ambapo hadi Juni 2022, Vyama Vikuu vya Karagwe District Cooperative Union – KDCU, Kahama Cooperative Union – KACU, Chato Cooperative Union – CCU na Umoja Liwale vimeanzisha kampuni kwa ajili ya biashara za mazao.

UANZISHWAJI WA BENKI YA TAIFA YA USHIRIKA

Amesema tume imeratibu uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ambayo itamilikiwa na Vyama vya Ushirika kwa asilimia 51 na taasisi na watu binafsi watamiliki kwa asilimia 49.

Amesema lengo la kuanzishwa Benki hiyo ni kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa wanachama.

Amesema benki hiyo inatarajiwa kuzinduliwa itakapokidhi kigezo cha kuwa na mtaji wa Shilingi Bilioni 15.

“Hadi sasa benki hii mtaji wake umefikia Shilingi Bilioni 3.7. Tume inaendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika na wadau wengine kununua hisa katika Benki hiyo,”amesema.

AJIRA NA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA KIJAMII KATIKA VYAMA

Mkurugenzi huyo amesema kuongezeka kwa uwekezaji katika vyama vya Ushirika kumesababisha ongezeko la ajira kutoka 100,100 mwaka 2020/2021 hadi 146,555 mwaka 2021/2022.

Amesema kati ya ajira zilizopatikana, za kudumu ni 31,819, za mkataba ni 28,990 na za msimu ni 85,746.

Aidha Vyama vya Ushirika vimekuwa chachu ya wananchi kupata huduma za kijamii ambapo kwa sasa vimeanza kutoa huduma ya Bima ya Afya kwa wanachama wake kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

About the author

mzalendoeditor