Featured Kitaifa

TMDA YAWAASA WAFUGAJI KUACHA KUNUNUA DAWA ZA MIFUGO KWENYE MINADA NA MAGULIO

Written by mzalendoeditor

 MENEJA wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ( TMDA) Kanda ya Kati, Bi. Sonia Mkumbwa,akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la TMDA katika Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Kilimo ni biashara,shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo,Uvuvi na Mifugo”yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni  kanda ya kati Jijini Dodoma.

MKAZI wa Dodoma Bw.Mohamed Makunzo,akiuliza maswali mara baada ya kutembelea banda la TMDA katika Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Kilimo ni biashara,shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo,Uvuvi na Mifugo”yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni  kanda ya kati Jijini Dodoma.

MCHUNGUZI wa Dawa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ( TMDA) Kanda ya Kati Bw.James Tanguye,akimpa elimu Mkazi wa Dodoma Bw.Mohamed Makunzo,ambaye alifika katika banda la TMDA kupata elimu zaidi wakati wa Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Kilimo ni biashara,shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo,Uvuvi na Mifugo”yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni  kanda ya kati Jijini Dodoma.

MENEJA wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ( TMDA)  Kanda ya Kati, Bi. Sonia Mkumbwa,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la TMDA katika Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu ‘Kilimo ni biashara,shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo,Uvuvi na Mifugo”yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni  kanda ya kati Jijini Dodoma.

.  ……………………….. 

Na Alex Sonna-DODOMA

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa wito kwa wafugaji kuacha kununua dawa za mifugo kiholela katika minada na magulio ili kuepuka kuuziwa dawa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi kwani kunahatarisha afya za mifugo yao na afya za walaji.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Bi. Sonia Mkumbwa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika banda la Mamlaka hiyo katika maonesho ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya nanenane – Nzuguni Jijini Dodoma.
Aidha, Bi. Mkumbwa amebainisha kuwa TMDA ina jukumu la kuhakikisha kuwa bidhaa za dawa zikiwemo za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi vina ubora kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kimataifa na kitaifa kwa kufanya usajili wa bidhaa hizo, ukaguzi wa viwanda na maeneo ya kutolea bidhaa hizo ili kuendelea kumlinda mwananchi.
“TMDA inahakikisha inafuatilia ubora wa bidhaa hizo mara kwa mara katika soko kwa kufanya kaguzi katika maeneo ya kuzalishia, kutunzia na kuuzia ili kuhakikisha matoleo yaliyopo katika soko yanakidhi vigezo ikiwapo kufanya uchunguzi wa kimaabara. Lakini pia maabara yetu imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na endapo mamlaka itabaini kuna bidhaa zisizo na ubora basi hatua za kisheria huchukuliwa kwa waliokiuka ikiwemo uteketezaji wa bidhaa hizo pamoja na tozo za faini kwa mujibu wa Sheria”, Amesema meneja huyo.
Vilevile, amesema TMDA inaendelea kufuatilia usalama wa bidhaa inazodhibiti na inatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa endapo watapata madhara yoyote kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.
TMDA Kanda ya Kati imeshiriki katika maonesho ya Sikukuu ya wakulima na wafugaji (nanenane) kwa lengo la kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya bidhaa inazozidhibiti kwa wananchi hususan wafugaji ili kuendelea kulinda afya ya jamii na kuleta tija katika uchumi wa taifa.

About the author

mzalendoeditor