Featured Kitaifa

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WASICHANA KUTOKUBAGUA MAFUNZO YA UKUZAJI UJUZI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifurahi jambo na kijana mnufaika wa fani ya ufundi Uashi, Grace William wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo, katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA, mkoani Kigoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akiangalia unifomu iliyoshonwa na wanagenzi wa fani ya ushonaji alipofanya ziara katika chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na vijana wa fani ya ufundi viyoyozi na majokofu wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA, mkoani Kigoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifurahi na kucheza pamoja na wanagenzi nyimbo ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa ufadhili wa mafuno hayo ya programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.

PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

*************************

Na: Mwandishi Wetu – KIGOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka wasichana kuacha mtazamo hasi wa kubagua fani za ujuzi zinazotolewa kwa madai kwamba ni za wavulana.

Ameeleza hayo wakati wa ziara yake katika Chuo cha ufundi stadi VETA, mkoani Kigoma alipotembelewa wanagenzi katika chuo hicho kwa lengo la kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.

Waziri Ndalichako alisema kuwa mwitikio wa vijana katika kushiriki kwenye mafunzo ya ukuzaji ujuzi ni mkubwa lakini idadi ya wasichana kwenye baadhi ya fani ni ndogo kutokana na mtazamo hasi kuwa baadhi ya fani ni kwa ajili ya wavulana.

“Nimefurahi kuona vijana wamekuwa na mwitikio chanya na wamejitokeza kwa wingi sana kupata ujuzi na tumeshuhudia kwenye baadhi ya fani ambazo zimekuwa zikihusisha wavulana pekee hivi sasa hata wasichana wanaweza kufanya,”

Aidha, Mheshimiwa Ndalichako alitoa wito kwa vijana wa kike kutobagua fani za stadi za kazi zinazotolewa kuwa ni kwa ajili ya wavulana pekee baadala yake wajenge ujasiri wa kuchangamkia fursa zinapojitokeza ili wajikwamue kiuchumi.

Sambamba na hayo Waziri Ndalichako alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni tisa kwa ajili ya kugharamia mafunzo yanayotolewa kupitia programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo itawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na hatimaye kujiajiri, kuajiriwa ama kuajiri wenzao.

“Dhamira ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ni kuona vijana wanajikwamua kiuchumi kwa kupata ujuzi ambao utawawezesha kufanya kazi ambazo zinatija kwa nchi yetu hivyo, niwasihi vijana wa kike, kiume na wenye ulemavu kuchangamkia fursa ambazo serikali inazitoa ili wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo ya taifa,” alisema Waziri Ndalichako

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Kigoma, Bw. Paul Kimenya, alieleza kuwa chuo hicho ni miongoni mwa vyuo 62 nchini vilivyopewa jukumu na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa mafunzo kwa vijana ambayo yamewezakuwajengea vijana hao mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka katika kutoa huduma mbalimbali kama vile kutoa huduma za kiufundi ndani na nje ya chuo hicho.

Naye Mnufaika wa Mafunzo hayo, Farida Misana ameshukuru Serikali kwa ufadhili wa mafunzo hayo ambayo yamewasaidia vijana kupata mwangaza wa kutambua mchango walionao katika jamii zao kwa kuweza kujiajiri na pia kuondokana na utengemezi.

About the author

mzalendoeditor