Featured Kitaifa

DC MWANAHAMISI AHAMASISHA WOTE KUHESABIWA

Written by mzalendoeditor

Na Alex Sonna-DODOMA

MKUU wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuibeba kauli mbiu ya Sensa ya watu na makazi yam waka 2022,jiandae kuhesabiwa ili kila mtu aweze kuhesabiwa mahali atakapoamkia siku ya zoezi hilo Agosti 23,2022.

Aidha,amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutowaficha watu wenye ulemavu na wageni watakaolala usiku wa kuamkia siku ya sensa.

Akizungumza na Mzalendo Blog Leo Agosti 5,2022,Mkuu huyo wa wilaya amesema zoezi hilo ni muhimu hivyo ni vyema kila mtu bila ya kujali umri,jinsia wala hali aliyonayo anapaswa kuhesabiwa.

“Tanzania kama nchi inatekeleza wajibu wa kushiriki zoezi la sensa ili kutambua idadi ya wananchi wake,rika zao,hali zao za kiuchumi,aina ya watu kama ni wenye ulemavu ama la,”

“Kutokana na umuhimu huu sote kwa pamoja tushiriki,tunaona halmashauri zinatoa mikopo kwa wanawake,vijana na wenye ulemavu,ili kuleta ufanisi kwenye utoaji wa mikopo hii ni muhimu kujua idadi yetu,”ameongeza.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi ambazo zimesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo wilayani Bahi.

“Wana Bahi ni lazima tumuunge mkono Rais wetu Samia, ni lazima tutoke tuhesabiwe,ni vyema tushiriki zoezi hili,hata katika kaya mama ama baba ni lazima ajue idadi ya watu wake ili aweze kukidhi mahitaji yao,”amesema.

Amesema katika kuhamasisha zoezi hilo la sensa wilaya ya Bahi wanaendelea na ligi ya sensa inayoshirikisha timu 16,lakini pia wanakuja na marathon ya sensa lengo la kufanya hivyo ni kuwaweka tayari wananchi kuhesabiwa.

About the author

mzalendoeditor