Featured Kitaifa

SH.BILIONI 1.1 ZAKUSANYWA KAMPENI GGM KILI CHALLENGE 2022

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai (kulia) akipokea bendera kutoka kwa mmoja wa washiriki wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangia fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi. Kulia kwake ni Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo. Hafla ya mapokezi hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika lango la Mweka Moshi.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai (wa pili kulia) pamoja na Mkuu wa mkoa wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule (katikati) wakipokea bendera kutoka kwa mmoja wa washiriki wa kampeni ya GGM Kili Challenge waliopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangia fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda na nyuma yao aliyevaa kofia ni Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo. Hafla ya mapokezi hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika lango la Mweka Moshi.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangia fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi. Hafla ya mapokezi hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika lango la Mweka wilayani Moshi.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo akimpongeza mmoja wa washiriki wa kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangia fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi. Hafla ya mapokezi hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika lango la Mweka wilayani Moshi.

…………………………………..

NA MWANDISHI WETU-

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS), imeendelea kuweka rekodi utoaji wa huduma za kijamii baada ya kukusanya zaidi ya Sh bilioni 1.1 kupitia kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 iliyoanza Juni 29 na kuhitimishwa Julai 21 mwaka huu.

Kampeni hiyo iliyoasisiwa na GGML miaka 20 iliyopita, ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu VVU/Ukimwi pia kuchangisha fedha za udhibiti wa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa lengo la kusaidia jitihada Serikali kufikia sifuri tatu kwa maana ya kutokomeza maambukizi mapya kwa kufikia asilimia sifuri, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Moshi katika hafla ya mapokezi ya washiriki 52 ambao kati yao 24 walipanda mlima Kilimanjaro kwa kutembea kwa miguu na 28 kwa kuuzunguka kwa kutumia baskeli kupitia lango la Machame na kushukia Mweka, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simona Shayo alisema kampeni ya mwaka huu imekuwa na mafanikio ya kipekee.

Alisema kampeni hiyo iliyozinduliwa rasmi Juni 29 jijini Dodoma na kufuatiwa na harambee ya uchangiaji fedha iliyofanyika Julai 14 kisha Julai 15, 2022 washiriki wakaagwa kwa ajili ya zoezi hilo la kupanda mlima, pia ilihusisha utoaji wa huduma bure za upimaji wa VVU na kisukari na utoaji wa chanjo ya UVIKO -19 kwa wakazi wa Mji wa Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

Alisema huduma hizo zilianza kutolewa katika lango la Machame, Kialia, Soko la Kalali na Nshara na sasa Mweka.

 “Ni furaha kubwa kuwaeleza kuwa katika huduma hizo zilizoanza kutolewa kuanzia tarehe 15 hadi 18 Julai mwaka huu, jumla ya watu 463 wamepimwa VVU ambapo wote majibu yameonesha hawana maambukizi ya VVU. Vivyo hivyo watu 411 wamejipima wenyewe kwa hiari. Hii ni hatua kubwa katika muitikio wa Watanzania kutaka kujua hali ya afya zao,” alisema.

Pia alisema katika utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19, watalaam wamefanikiwa kutoa chanjo kwa watu 822 ambao kati yao wanaume ni 365 na wanawake ni 427 wakati katika uchangiaji wa damu zimekusanywa chupa au unit 27 za damu ilihali katika zoezi la ugawaji wa kondomu, jumla ya mipira ya kiume 9,335 na ya kike 200 imegawiwa katika maeneo hayo.

 “Pia ili kutoa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu masuala ya VVU/Ukimwi, tembe za PrEP ambazo ni mahsusi kwa matumizi ya kupunguza makali ya VVU na kwa watu wasio na VVU ili kuzuia upatikanaji wa maambukizi ya VVU ziligawiwa pamoja na vipeperushi 204 vya masuala ya afya ya uzazi,” alisema.

Aidha, Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko alisema fedha zilizokusanywa kwenye kipindi cha kampeni hiyo kwa ujumla ni Sh bilioni moja.

 Pia alitoa wito kwa wadau wengine kukaa mezani na taasisi hiyo ili kupeana mbinu za kuchangisha fedha zaidi kutunisha mfuko wa udhibiti Ukimwi nchini.

Aidha, akizungumza katika mapokezi hayo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai aliwapongeza washiriki hao 52 wa waliopanda Mlima Kilimanjaro na kuwaitwa kuwa ni mashujaa.

 Aidha, akizungumzia matokeo ya vipimo vya VVU kwa watu zaidi ya 400, Kagaigai alisema yanaonesha jinsi gani mapambano wanayofanya kukabiliana na VVU sasa yanaelekea kwenye mafanikio.

 Mkuu wa mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule naye alipongeza juhudi zilizooneshwa na GGML na wadau wake na kusema kuwa matokeo ya vipimo hivyo  yanaonesha dhamira ya serikali kufikia sifuri tatu inaenda kutimia.

Aidha, alionya changamoto iliyobaki ni ya maambukizi mapya kwa kuwa waathiriwa wengi hawapotezi maisha kwa VVU au hawaoneshi dalili.

 Aidha, mmoja wa wapanda mlima huo, Lucina Livigha alisema licha ya changamoto za upandaji wa mlima, wamejihisi fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya kampeni hiyo inayookoa maisha ya Watanzania.

About the author

mzalendoeditor