Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AUNGANA NA WAUMINI KATIKA IBADA YA MISA TAKATIFU MPANDA MKOANI KATAVI

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango akishiriki ibada ya misa takatifu  katika Kanisa kuu katoliki la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Jimbo la Mpanda mkoani Katavi leo tarehe 24 Julai 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango akizungumza na waumini mara baada ya kushiriki ibada ya misa takatifu katika Kanisa kuu katoliki la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Jimbo la Mpanda mkoani Katavi leo tarehe 24 Julai 2022.

************************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 24 Julai 2022 ameungana na waumini wa Jimbo Katoliki la Mpanda mkoani Katavi katika ibada ya misa takatifu katika Kanisa kuu katoliki la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ibada ilioongozwa na padri Filbert Bafumkeko.

Akizungumza na waumini mara baada ya kumalizika kwa misa hiyo, Makamu wa Rais amewahakikishia waumini na watanzania kwa ujumla nia ya dhati ya serikali ya awamu ya sita katika kuwaletea wananchi maendeleo na kujitahidi kadri iwezekanavyo kuhakikisha taifa linasonga mbele. Aidha Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa mkoa huo kwa maendeleo katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, maji na miundombinu.

Makamu wa Rais amewashukuru waumini kwa maombezi yao na kuwaomba kuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya ndoa katika umri mdogo ambazo zimekua changamoto kubwa ya mkoa huo. Amesema zipo athari mbaya zinazotokana na mimba katika umri mdogo ambazo ni pamoja na kifo na maradhi ya fistula. Amewaasa kuhakikisha watoto wanapata elimu ili mkoa huo uendelee kutoa viongozi wa kitaifa na wataalamu mbalimbali kwa manufaa ya taifa.

Aidha Makamu wa Rais amewataka waumini hao na wananchi wa Katavi kwa ujumla kuweka akiba ya chakula ambacho wamefanikiwa kupata katika mkoa huo licha ya upungufu wa mvua uliojitokeza mwaka huu. Pia amesisitiza suala la upatikanaji wa lishe kwa wananchi wa mkoa huo ambao unazalisha chakula kwa wingi kutokana na kiwango cha udumavu kinachojitokeza katika mikoa ambayo ina uzalishaji mkubwa wa chakula.

Kwa upande wake Padri Filbert Bafumkeko amesema waumini wakatoliki mkoani Katavi wakiungana kwa pamoja wanaouwezo wa kuibadili jamii ya mkoa huo na  kuondokana na suala la ongezeko la mimba katika umri mdogo kutokana na idadi kubwa ya waumini waliopo katika eneo hilo.

Makamu wa Rais amemaliza ziara ya kikazi mkoani Katavi ambapo amekagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero na changamoto za wananchi katika mkoa huo.

About the author

mzalendoeditor