Katibu Mkuu wa Chama Cha Askari Wastaafu waliopigana vita kuu ya Pili ya Dunia ( wa pili kulia) na Mzee Omary Shangazi mwenye umri wa miaka 103 ambaye pia amepigana vita hivyo na kurudi salama ( wa pili kushoto) walivyotembelea viwanja vya mashujaa kukagua maandalizi kuelekea sherehe za siku ya mashujaa yatakayofanyika kitaifa Julai 25,2022 jijini Dodoma
…………………………………..
Na Okuly Julius-Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Askari Wastaafu waliopigana vita kuu ya Pili ya Dunia TLC, Charles Lubala amesema kuwa wamefurahishwa na kurudishwa kwa maadhimisho ya sherehe ya siku ya mashujaa kwani imekaa zaidi ya miaka mitano bila kuadhimishwa.
Lubala amemshukuru Mhe.Rais Samia kwa kurudisha maadhimisho hayo ikiwa ni fahari kubwa kwao kama mashujaa waliolipigania taifa tangu enzi za vita vya pili vya dunia huku akisema kuwa Mhe.Rais ameonesha kuwajali na kuthamini juhudi zao ndio maana akaamua kurudisha sherehe hizo.
“Kiukweli sisi kama chama cha maaskari wastaafu waliopigana vita kuu ya pili ya dunia ya mwaka 1949-1945 tumefarijika sana kuona Mhe.Rais Samia amerudisha tena hii siku ambayo itaadhimishwa kila mkoa ila kitaifa itafanyika hapa jijini Dodoma “amesema Lubala
KUTANA NA MZEE OMARY SHANGAZI MWENYE UMRI WA MIAKA 103 ALIYEPIGANA VITA KUU YA PILI YA DUNIA
Kutoka katika Uwanja wa Mashujaa Jamatini Jijini Dodoma Kwenye maandalizi ya Maadhimisho ya siku ya mashujaa MZALENDO BLOG Imefanya mazungumzo na Mzee Omary Shangazi mwenye umri wa miaka 103 ambaye ameshiriki vita kuu ya Pili ya Dunia vilivyopigwa kuanzia mwaka 1939 Hadi 1945 kati ya Ujerumani,Itali,Japani na Mataifa yaliyoshikamana nazo(Bulgaria na Hungari) dhidi ya Nchi nyingi za Dunia ziliitwa Mataifa ya ushirikiano ambazo ni Uingereza,Uchina,Urusi na Marekani
Mzee Omary ameeleza namna ambavyo alivyoshiriki vita hivyo mpaka kurudi nyumbani salama huku akiwa amewapoteza rafiki zake wengi ambao baadhi Yao waliuawa Kwa kulipuliwa na Bomu kwenye meli na Dikteta wa Kinazi Adolf Hitler wakati walipokuwa wanaelekea kwenye misheni za kivita.
“Nimewapoteza rafiki zangu wengi Sana wengine walitunguliwa ndani ya meli wakati wakienda Misiri kwenye Misheni umati wa watu wakazamishwa”amesema Mzee Omary Shangazi
Mzee Omary ambaye ni mkazi wa Arusha amesema kuelekea sherehe ya siku ya mashujaa anaiomba serikali iwaenzi na kuwapa heshima yao kwani ndio waliopigania taifa hili.
“Sisi kama Veterans tulisahaulika sana lakini namshukuru Mhe.Rais Samia kwa kutukumbuka tena na kuamua kurejesha maadhimisho haya na kwa hili nampongeza sana na niwaombe wanadodoma kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 25,2022 kushuhudia sherehe hizi”amesema mzee Omary