Featured Kitaifa

SERIKALI KUTUMIA SH.BILIONI 700 KUHAMISHA WANANCHI NDANI YA ENEO LA NGORONGORO

Written by mzalendoeditor
NAIBU Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayeshughulikia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii DK.Christopher Timbuka ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 22,2022 jijini Dodoma kuhusu  utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayeshughulikia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii DK.Christopher Timbuka ,leo Julai 22,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu  utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa taarifa ya utekelezaji ya Mamlaka ya Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 leo Julai 22,2022 jijini Dodoma.
…………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI inatarajia kutumia shilingi bilioni 700 kutekeleza zoezi la kuwahamisha wananchi wa vijiji 25 vilivyomo ndani ya eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha.
Kauli hiyo imetolewa  leo Julai 22,2022 jijini Dodoma na  Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayeshughulikia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii DK.Christopher Timbuka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23
Dk.Timbuka amesema kuwa mpaka  sasa zaidi ya kaya 700 zenye wakazi 4344 zikiwa tayari zimejiorodhesha kwa hiari kuhamia katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoani Tanga.

 

“Hadi sasa kasi ya wananchi kuhama inazidi Kuongezeka ambapo mpaka sasa kuna Kila sababu ya kuongeza miundombinu kwaajili ya wananchi hao,eneo hilo ni rafiki sana kwa shughuli za kibinadamu,”amesema.

Amesema kuwa kuna sababu mbalimbali zilizoisukuma serikali kuwaahamisha wananchi kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro ni  kulinda eneo hilo kutokana na takwimu zilizofanywa na ofisi ya taifa ya takwimu NBS imeonekana kuwa kuna kiwango kikubwa sana cha umasikini.
“Asilimia 64 ya wakazi wanaoishi katika hifadhi ya taifa ya Ngorongoro hawajui kusoma wala kuandika na hii inasababishwa na kuhofia kwenda shule kutokana na wanyama wakali ,huku wengine wanashindwa kufanya shughuli zao za ufugaji kutokana na kushambuliwa na wanyama wengine wanapoteza maisha kabisa”Amesema Dk.Timbuka
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa, amesema kuwa wananchi waliohama kabla ya uamuzi wa serikali ya awamu ya sita wa kuhifadhi eneo la Ngorongoro lililohifadhiwa kisheria tangu mwaka 1959 amesema kuwa ni bahati kubwa kwa hawa wanaohama kwa sasa kwani serikali imewekeza fedha kubwa kwa ajili ya kuwaandalia mazingira ya kuhamia.
“Ni bahati kubwa yaani unahama alafu unakuta nyumba ipo kwenye eneo la ekari mbili na nusu alafu una shamba la ekari tano umepewa bure na serikali yako sikufu inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan tuseme tu kwamba hawa wananchi wa Ngorongoro wana bahati kubwa na niwaombe tu watumie hii bahati vizuri”Amesema Msigwa

About the author

mzalendoeditor