Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS DK.MPANGO ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WIZARA YA NISHATI

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini na Chama wakati alipowasili katika Uwanja wa Shule ya Msingi Inyonga Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kuzungumza na wananchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango akicheza wimbo maalum wa kushiriki sensa ya watu na makazi ukiimbwa na kwaya ya Agape kutoka katika kikundi cha Upendo cha Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi wakati alipofika kuzungumza na wananchi wa Wilaya hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango akicheza wimbo na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Inyonga iliopo  Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi wakati alipofika kuzungumza na wananchi wa Wilaya hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi pamoja na wananchi wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi wakati wa ziara yake katika mkoa hu oleo

…………………………………

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango ameigiza Wizara ya Nishati kuhakikisha ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme wa Gridi ya Taifa cha Inyonga kukamilika ifikapo Oktoba mwaka 2023 na mkoa wa Katavi unaunganishwa katika Gridi ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi  mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa  msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi katika eneo la Inyonga Wilaya ya Mlele. Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao umechelewa kwa takribani miezi nane mpaka sasa.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka wakurugenzi kuacha mara moja tabia ya kutoza ushuru kwa mazao yanayosafirishwa chini ya tani moja kwani serikali ilionmdoa tozo hizo ili kuwasaidia wakulima wadogo kupata kipato. Amesema wakurugenzi wanapaswa kutafuta mbinu sahihi za kuwabaini wanaokusanya mazao zaidi ya tani moja ili kuwanusuru wale wakulima wadogo.

Pia Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Mlele kuendelea kutafuta elimu kuhusu lishe ili wananchi wa mkoa huo wawe na afya bora kulingana na mazao mengi wanayozalisha. Makamu wa Rais amewataka kuendelea na juhudi za kutunza mazingira ikiwemo kupiga vita uchomaji miti na uchafuzi wa mazingira. 

Makamu wa Rais amewaagiza wazazi na walezi mkoa wa Katavi  kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ili taifa kuwa na rasilimali bora zaidi itakayoharakisha maendeleo.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Mwamvua Mrindoko ameishukuru Serikali kwa kuuwezesha mkoa huo kwa miradi mbalimbali inayochochea maendeleo kama vile miradi ya elimu, maji, barabara, afya pamoja kuongezewa idadi ya watumishi wapatao 692 katika sekta ya afya na elimu kwa mara moja.

Aidha Mkuu wa Mkoa amemueleza Makamu wa Rais maendeleo ya sekta ya kilimo mkoani Katavi iliopelekea kupatikana kwa mazao ya kutosha. Amesema jumla ya tani zaidi ya laki tisa za mazao ya chakula zimevunwa mwaka huu na kufanya ziada ya chakula kuwa tani  zaidi ya laki tano  katika mkoa huo. Amewaasa wazazi na walezi kuendelea kuweka akiba ya chakula pamoja na kuhakikisha biashara ya mazao inatumika kuhudumia watoto wao katika kupata elimu na mahitaji muhimu.

Awali akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mlele, Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Isaac Kamwele ameiomba serikali kukamilisha ujenzi wa majosho sita ili kuwasaidia wananchi wa eneo hilo ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji. Pia ameongeza kwamba kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wananchi wananchi hao wanahitaji shule mbili zaidi za elimu ya msingi pamoja na Chuo cha Veta kitakachowasaidia katika kupata ujuzi.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo ziarani mkoani Katavi ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

About the author

mzalendoeditor