Featured Kitaifa

MHANDISI LUHEMEJA :NARCO KUANZA OPERESHENI MAALUM KUUNUA MIFUGO

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Joseph Mkirikiti akizungumza jana ofisini wakati wa kikao na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) waliopo Rukwa kwa ajili ya maandalizi ya operesheni maalum ya kununua mifugo.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa taarifa kwa viongozi wa mkoa wa Rukwa jana mjini Sumbawanga kuhusu maandalizi ya operesheni maalum ya kununua mifugo toka kwa wananchi kwa ajili kuhifadhi katika ranchi ya Kalambo itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu .
Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

…………………………………

Na OMM Rukwa

Serikali imesema itaanzisha operesheni maalum ya kununua mifugo toka kwa wafugaji kwa ajili ya kuimarisha ranchi ya taifa ya Kalambo kuwa na mifugo bora itakayotumika kuongeza thamani pamoja na kuuza bidhaa za mifugo kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja jana (19.07.2022) alipozungumza na viongozi wa Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga akiwa katika ziara ya kukagua maandalizi ya operesheni hiyo inayotegemewa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Rachi za Taifa aliongeza kusema lengo la serikali ni kufanya operesheni ya kununua mifugo ya wananchi ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo ambao watapelekwa katika ranchi ya Kalambo iliopo mkoani Rukwa ili kuwezesha serikali kwa na hifadhi ya mifugo  huku wananchi wakipata fedha za uhakika   hatua itakayokuza sekta ya mifugo kuchangia pato la taifa.

“Tunataka mkoa wa Rukwa uwe ni hifadhi (reserve) ya mifugo ambapo eneo la hekta 62,000 za rachi ya Kalambo itatumika kuongeza thamani ya mifugo itakayonunuliwa toka kwa wafugaji wa mikoa yote nchini kwani takwimu zinaonesha Tanzania kuna ng’ombe wapatao milioni 32 lakini wametawanyika  bila utaratibu” alisisitiza Mhandisi Luhemeja.

Alitaja mkakati mwingine wa NARCO ni kuona ranchi ya Kalambo inakuwa na ng’ombe Milioni Moja ifikapo mwaka 2023 ili Tanzania iweze kufungua masoko ya bidhaa za mifugo ikiwamo nyama bora na ngozi hatua itakayowezesha taifa kupata mapato ya uhakika na kuleta mapinduzi kwenye sekta ya mifugo.

Mhandisi Luhemeja alitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na viongozi wengine kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi wenye mifugo itakapozinduliwa operesheni hii kuuza mifugo yao kwa serikali ili wapate fedha  pia kuweza kuwa na mifugo inayolingana na maeneo wanayoishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alipongeza hatua hiyo ya serikali kupitia NARCO kuwa itakuwa na faida kwa wananchi wenye mifugo mingi pia itasaidia kuondosha migogoro baina ya wakulima na wafugaji kutokana na mlundikano wa mifugo kwenye maeneo karibu wa mashamba.

Mkirikiti alibainisha kuwa “ haiwezekani kuwambia wafugaji wapunguze mifugo wakati hakuna mahala tunapowaelekeza wakauze , hivyo uamuzi wa serikali kuanzisha operesheni ya kununua mifugo na kuitunza katika ranchi ya Kalambo utakuwa na tija kwa wananchi na kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji “ alisema Mkirikiti.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alisema Rukwa  ina fursa kubwa ya kutumia soko la nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi kuuza bidhaa za mifugo na kilimo kutokana na uwepo wa bandari za Kasanga, Kipili na Kabwe katika Ziwa Tanganyika hivyo ranchi ya Kalambo itakapo anza kuzalisha kwa wingi bidhaa za mifugo itapata uhakika wa soko.

About the author

mzalendoeditor