Featured Kitaifa

VYAMA VIKUU VYA USHIRIKA VYA PAMBA MIKOA YA SHINYANGA NA GEITA VYAISHUKURU SERIKALI, BENKI YA TADB KUFUFUA VIWANDA VYA PAMBA

Written by mzalendoeditor


Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU), Benedicto Bulugu Ngunda akionesha pamba inayochambuliwa katika kiwanda cha MBCU
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Vyama Vikuu vya Ushirika vya Pamba vya mikoa ya Shinyanga na Geita vimeishukuru Serikali kwa uanzishwaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (Tanzania Agricultural Development Bank – TADB) ambayo imevipa mikopo iliyofufua viwanda vya kuchambua pamba ambavyo vilikuwa vimesimama kwa miaka mingi na sasa vinafanya kazi ya kununua na kuchambua pamba kutoka kwa wakulima wa maeneo hayo na mikoa jirani kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki hii na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania waliotembelea Vyama hivyo vya Ushirika, Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika wamesema Benki ya TADB imeleta furaha kwa wakulima wa zao la pamba kwani mazao yao yananunuliwa na uchambuzi wa pamba unaendelea kwenye viwanda vyao.
 
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU), Benedicto Bulugu Ngunda amesema serikali inavithamini na kuvipa kipaumbele Vyama Vikuu vya Ushirika ndiyo maana kupitia Benki ya TADB imewezesha upatikanaji wa mikopo ili kufufua viwanda vya kuchambua pamba vilivyokuwa havifanyi kazi.
 
 
“Serikali inatuthamini imewezesha upatikanaji wa fedha kupitia Benki ya TADB, na kwa kweli benki hii imekuwa bega kwa bega na sisi kwani wanatushauri,wanatuamini na wanatupatia fedha kwa wakati na wanachama wetu pamoja na wakulima kwa ujumla wamepata hamasa kubwa ya kuendelea kulima pamba kwani uhakika wa pamba yao kununuliwa upo”,amesema.
 
 
“Hivi sasa ile dhana ya Dhahabu nyeupe imerejea kwa kishindo, pamba ina thamani na bei imeongezeka. Hali kadhalika pamba inayozalishwa ina ubora mkubwa na wananchi hawachafui tena pamba kama zamani kwa kuweka maji, mchanga,mawe na vitu vingine, wameridhika na bei ya pamba”,ameeleza Bulugu.
 
 
Amesema msimu huu mwamko kwa wakulima wa pamba umeongezeka na sasa wanaendelea kukusanya pamba kutoka kwenye AMCOS 87 zenye wakulima 12,000 kutoka mkoa wa Geita na mikoa jirani ikiwemo Kigoma, Mwanza na Shinyanga.
 
 
Bulugu ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kuwahisha pembejeo kwa ajili ya kilimo cha msimu ujao hasa mbegu na viuatilifu kwani mdudu ‘Chawajani’ anashambulia mmea ukiwa mdogo hivyo ni vyema maandalizi ya kukabiliana na mdudu huyo yafanyike mapema kwa kuleta viuatilifu vinavyoua wadudu hao na wakulima wapewe kwa wakati.
 
 
Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Chato (Chato Co operative Union – CCU), Gereoni Gervas Chandika amesema mkopo kutoka Benki ya TADB umewezesha kufufuliwa kwa kiwanda chao ambacho hapo awali walikuwa wanakikodisha kwa watu binafsi.
 
 
Amesema hivi sasa ununuzi na uchambuaji wa pamba unaendelea kwani fedha zipo na wanaendelea kusomba pamba na kulipa madeni kwenye vyama vya msingi (AMCOS) walikonunulia pamba zoezi ambalo litahitimishwa ndani ya wiki mbili na kisha kuendelea na ununuzi wa pamba kwa bei itakayokuwepo ambayo haitapungua kwa bei elekezi ya serikali shilingi 1560 kwa kilo moja ya pamba.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Khamis Majogolo amesema baada ya kufufua kiwanda chao kupitia Mkopo wa Benki ya TADB , wanaendelea kununua na kuchambua pamba huku akibainisha kuwa mwaka huu wamepata pamba safi sana kutokana na maandalizi mazuri ya pamba kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).
Hata hivyo Vyama Vikuu vya Ushirika vya Pamba vya mikoa ya Shinyanga na Geita vimesema vinaendelea na mipango yake ya kuanzisha viwanda vya kusindika mafuta ya pamba kwani wamechambua mbegu za kutosha ili kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU), Benedicto Bulugu Ngunda akionesha pamba inayochambuliwa katika kiwanda cha MBCU. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Pamba ikiendelea kuchambuliwa katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU).
Kazi ya kulisha pamba kwenye mitambo kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU).
Muonekano wa sehemu ya mitambo ya kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU).
Zoezi la kupaki pamba kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU) likiendelea
Muonekano wa sehemu ya maghala ya kuhifadhia pamba kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (Mbogwe & Bukombe Co operative Union – MBCU).
Muonekano wa sehemu ya Kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Chato (Chato Co operative Union – CCU).
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Chato (Chato Co operative Union – CCU), Gereoni Gervas Chandika akielezea namna wanavyonunua na kuchambua pamba katika kiwanda chao cha CCU.
Uchambuzi wa pamba ukiendelea katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Chato (Chato Co operative Union – CCU).
 Muonekano wa sehemu ya mitambo ya kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Chato (Chato Co operative Union – CCU).
Muonekano wa sehemu ya mbegu za pamba zilizochambuliwa kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Chato (Chato Co operative Union – CCU).
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Khamis Majogolo akielezea kuhusu zao la pamba na namna wanavyonunua na kuchambua pamba
Magari yakishusha pamba katika Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) Mjini Kahama
Mhandisi wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Himelius Magege akionesha pamba ndani ya kiwanda hicho.
Mhandisi wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Himelius Magege akionesha pamba iliyochambuliwa katika kiwanda chao.
 
Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
 

About the author

mzalendoeditor