Featured Kitaifa

SHAKA AKAGUA MIRADI PEMBA, AAHIDI CCM ITAWALINDA WABUNGE ,WAWAKILISHI NA MADIWANI.

Written by mzalendoeditor
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka (katikati) akisalimiana na Mwananchi wa jimbo la Gando vsiwani Pemba baada ya kumkabidhi baiskeli ya Kutembelea  iliyotolewa na Mbunge wa jimbo hilo Salim Mussa Omari (wa pili kulia). Shaka amemkabidhi baiskeli hiyo jana na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka (wa pili kulia) akikabidhi funguo ya gari la kubebea wagonjwa kwa mmoja ya wananchi wa Jimbo la Gando (wa pili kushoto). Shaka amekabidhi funguo za gari hilo jana likiwa limetolewa na Mbunge wa Jimbo la Gando, Salim Mussa Omari (wa kwanza kushoto) na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa.(
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Wete visiwani Pemba wakati wa mkutano wa hadhara uliondaliwa na Mbunge wa Jimbo la Gando Salim Mussa Omari pamoja na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mariam Thani Juma. Mkutano huo umefanyika jana katika Uwanja wa Mpira Kizimbani na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa Wilaya ya Wete.(Picha na Fahadi Siraji, CCM Makao Makuu)
……………………………….
 
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amekagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kisiwani Pemba na kuwahakikishia wananchi kuwa Chama kitaendelea kuwalinda wabunge , Wawakilishi na madiwani wake wanaotekeleza ahadi zao.
 
Akiwa katika ziara hiyo iliyoanza jana visiwani humo, Shaka amekagua miradi ya madarasa na kisima cha maji safi na salama katika Jimbo la Gando, miradi ambayo imewapunguzia adha wananchi ikiwemo ya kufuata maji  umbali mrefu.
 
Akizungumza katika mkutano wa Mbunge wa Jimbo hilo,uliofanyika kwenye Uwanja wa Mpira Kizimbami Shaka amesema utekelezaji wa Miradi ya maendeleo unaofanyika katika Jimbo hilo na maeneo mengine yanayoongozwa na wabunge na madiwani wa CCM.
 
Shaka amesema utekelezaji wa Miradi unaofanywa na viongozi wa CCM unalenga kutekeleza ahadi na kutatua changamoto za wananchi katika huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji.
 
Aidha, Shaka amewahakikishia wabunge na madiwani wanaotokana na CCM kwamba Chama kitaendelea kuwalinda dhidi ya yeyote anayetaka kuwavuruga na kusababisha washindwe kutekeleza majukumu yao.
 
Amesema wabunge na madiwani wanapaswa kuachwa watekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba mwanachama yeyote mwenye malengo ya kuomba uongozi asubiri wakati mwafaka unaoruhusiwa kisheria.
 
Awali baada ya kuwasili kisiwani humo, Shaka alizuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Dk. Omari Ali Juma, wilayani Chakechake na baadae kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar marehemu Maalim Seif Sharif Hamad lililopo Kijiji cha Mnyali, Mtambwe wilaya ya Were Mkoa wa Kaskazini Pemba.

About the author

mzalendoeditor