Featured Kitaifa

SHILINGI BILIONI 75 KUIMARISHA UPATIKANAJI UMEME SIMIYU

Written by mzalendoeditor

 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ikungulyabashashi iliyopo wilayani Bariadi ambayo imeunganishwa na umeme kupitia mradi wa REA III Awamu ya Pili wakifurahi na Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba baada ya kuona manufaa ya umeme unaowawezesha kuweka makambi ya kujisomea, kutumia vifaa vya tehama na kuwasaidia kwenye majaribio ya kisayansi.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akizungumza na wanachi katika Kijiji cha Momela wilayani Itilima mkoani Simiyu ambapo aliwaeleza kuhusu kazi zinazoendelea za usambazaji umeme vijijini pamoja na mpango wa Serikali wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia vijijini.

Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba akimwelekeza Bi.Agnes Doto, mkazi wa mtaa wa viwandani wilayani Bariadi jinsi, gesi ya mitungi inavyofanya kazi na faida atakazopata mama huyo baada ya kutumia nishati hiyo safi ikiwemo kujiepusha na magonjwa katika mfumo wa hewa.

……………………………

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba, ameeleza kuwa changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoani Simiyu imefanyiwa kazi na Serikali na sasa mkoa huo umepelekewa mradi wa shilingi Bilioni 75 ambao unahusisha ujenzi  kituo cha kupoza umeme pamoja na miundombinu ya kusafirisha umeme wa kV 220 ambao utatekelezwa kwa miezi 18.

Waziri Makamba alisema hayo tarehe 13 Julai, 2022 wakati alipokagua eneo kutakapojengwa kituo hicho cha kupoza umeme katika eneo la Imalilo wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

“Wizara na TANESCO tumeamua kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme kutoka Ibadakuli Shinyanga hadi Simiyu pamoja na kujenga kituo cha kupoza umeme kwa sababu kuna changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika, Simiyu ni Mkoa wa mkubwa wa uzalishaji, kuna viwanda vya pamba na migodi na uwekezaji mwingine unatarajiwa kufanyika lakini hakuna umeme wa uhakika hivyo mradi huu ukikamilika utatatua changamoto hii.”alisema Makamba.

Alieleza kuwa, mkandarasi wa mradi huo atapatikana ndani ya mwezi mmoja ambapo fedha za utekelezaji wa mradi huo zitatoka katika mradi ujulikanao kama Gridi Imara wenye shilingi Bilioni 500 ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kuongeza uwezo na uhakika wa upatikanaji umeme katika maeneo ambayo yana mahitaji ya umeme lakini hakuna umeme wa uhakika.

Kuhusu umeme vijijini alisema kuwa, mkoa huo wenye vijiji 470, tayari vijiji 269 vimeshasambaziwa umeme na vijiji 201 vilivyosalia tayari kuna wakandarasi wawili wanaoendelea na kazi ya usambazaji umeme.

Katika kuboresha usimamizi wa miradi ya umeme vijijini, Waziri Makamba alisema kuwa, ndani ya mwezi mmoja Serikali itaajiri vijana takriban 139 watakaosambazwa katika Halmashauri zote nchini ili wawe waratibu wa miradi ya REA katika maeneo hayo.

“Vijana hawa 139 kazi yao ni kufuatilia miradi imefikia hatua gani, mfano kama vifaa vya umeme vimefika katika maeneo yao, kama nguzo zimechimbiwa mashimo, kama zimesimamishwa na kama nyaya zimevutwa, vijana hawa watakuwa pia kiungo cha mawasiliano kati ya Wizara, Tanesco, viongozi wa Serikali na kisiasa pamoja na wadau wengine wanaohusika na miradi hii.” Alisema Makamba

Kuhusu upatikanaji wa nishati bora ya kupikia vijijini,  alisema kuwa, Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 10.5 ili kutekeleza mradi huo na kufanya kampeni kubwa ya kuhamasisha matumizi ya nishati bora ya kupikia pamoja na tafiti za kubaini nishati na mfumo sahihi wa kusambaza nishati hiyo maeneo ya vijijini ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Pamoja na kukagua miradi ya umeme, akiwa mkoani Simiyu, Waziri wa Nishati alitoa elimu kwa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia pamoja na kugawa kugawa mitungi ya gesi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

About the author

mzalendoeditor