Featured Kitaifa

TUKIO LA UKATILI LAWAFIKISHA WAZIRI DKT. GWAJIMA NA NAIBU WAKE KWA MUATHIRIKA

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWM, Dodoma

Tukio la mtoto wa miaka 05 (jina limehifadhiwa) aliyefanyiwa ukatili tangu Aprili mwaka huu jijini Dodoma na huku familia ikionekana kutofahamu vema mwenendo wa shauri hilo linalo mkabili mtuhumiwa aliyefanya tukio limechukua sura mpya kufuatia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima na Naibu wake Mwanaid Ali Khamis kufika Nyumbani kwa MUATHIRIKA kutaka kujua hatma yake.

Viongozi hao kwa pamoja leo Julai 12, 2022 wamefika katika Mtaa lilipotokea tukio hilo wakiwa wameambatana na kundi la Watanzania wazendo wanaojitokea katika kupamba na Vitendo vya ukatili nchini (SMAUJATA).

Akiwa eneo la tukio Waziri Dkt. Gwajima, amesema shabaha ya ziara hiyo ni kutembelea maeneo ambapo ukatili umetokea na kujua
ufahamu wa manusura wa ukatili juu ya mwenendo wa kesi za watuhumiwa.

Ameongeza kuwa katika tukio hilo imebainika kuwa, jitihada za Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano na SMAUJATA zimesaidia kufuatilia na kufahamu kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa Katikati ya Julai, 2022.

Aidha Dkt. Gwajima amesisitiza mshikamano wa jamii yote ya wapenda amani katika kutokomeza ukatili kwenye jamii hasa kwa watoto kwani jamii ndio inaweza kuamua vitendo hivyo Kutokomezwa kwa kuhakikisha Kila mtu anatimiza wajibu wake wa kutoa taarifa za viashiria au vitendo vya ukatili vinavyotokea.

“Niwaombe tushikamane katika jamii ukiona vitendo vya ukatili vinafanyika usiseme mimi hayanuhusu haya, yanatuhusu sote, maana na wewe unaweza ukafanyiwa au mwanao akapatwa na hayo tuchukue hatua tutoe taarifa tusikae kimya” alisema Dkt Gwajima

“Tumekuja hapa na Hawa wazalendo jasiri wanaojitolea katika kupambana na vitendo vya ukatili nchini na sisi tujitoze kuwakomboa Watoto na Wanawake wanaofanyiwa ukatili wa aina yoyote ile tuliokoe Taifa” alisisitiza Dkt Gwajima.

Akizungumza Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kuwa wepesi wa kuripoti viashiria au vitendo vya ukatili vinavyotokea kwenye mamlaka lakini waache mchezo wa kumalizana ndani ya jamii ambao unasababisha wanafanyiwa Vitendo hivyo kukosa Haki zao.

“Ndugu zangu huu mchezo tuuache tuwalinde Watoto wetu dhidi ya vitendo hivi kwani kumalizana kisa aliyefanya kitendo cha ukatili ni ndugu yako au mumeo wako hili hapana tutoe taarifa, na sisi kama Serikali tutachukua hatua” alisema Mhe. Mwanaidi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima na Naibu wake Mhe Mwanaidi Ali Khamis wakishirikiana na SMAUJATA wameanza kufuatilia Mtaa kwa Mtaa hali ya vitendo vya Ukatili kwa wanawake na watoto vinavyoonekana kushamiri ndani ya jamii.

About the author

mzalendoeditor