Featured Kitaifa

MAASKOFU AMECEA WAVUTIWA NA NEMC

Written by mzalendoeditor

Na Alex Sonna

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na mazingira, Dk.Selemani Jafo amelipongeza Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kutoa elimu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati.

Dk.Jafo ametoa pongezi hizo leo alipotembelea banda la NEMC lililopo kwenye maonesho ya kimataifa ya mazingira katika Mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu hao (AMECEA)unaofanyika kituo cha mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere mkoani Dar es salaam.

Ameishukuru NEMC kwa usimamizi wa Sheria za Usimamizi wa Mazingira na kuwaomba wadau kuzingatia sheria hizo ili kulinda mazingira ya nchi.

“Niishukuru taasisi yetu ya NEMC ule usimamizi wa sheria wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana nchini kwetu, kwa hiyo niwaombe sana wadau kushirikiana na taasisi zetu kwenye masuala ya mazingira, watambue wanapotimiza majukumu yao wanataka nchi iwe salama wakati wote,”amesema.

Amesema mkutano huo umekuja na ajenda mahsusi ya mazingira ili kuhakikisha yanatunzwa na kuchochea maendeleo endelevu ya dunia.

“Katika hili tumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ambayo yanaonesha namna Tanzania ilivyojidhatiti kulinda mazingira tukiongozwa na Sera yetu ya mazingira ya Mwaka 2021, ajenda ya mazingira ni mtambuka na sasa kumekuwapo na vikwazo vingi vya kimazingira.”

“Tumeshuhudia maeneo mengi sana kiwango cha bahari kinaongezeka, hali ya joto inaongezeka, ukame unashamiri kwenye baadhi ya maeneo hivyo tuna kila sababu ya kutunza mazingira,”amesema.

Ameagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha miji yote inaimarisha masuala ya usafi wa mazingira.

Kwa upande wake, Askofu kutoka Jimbo la Geita, Flavian Kassala ambaye ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesema elimu waliyopata ni msingi imara wa upangaji na utekelezaji wa shughuli za mendeleo kwa kuzingatia athari zinazoweza kutokea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Akitoa elimu kwa washiriki wa mkutano huo, Mtaalam kutoka NEMC, Suzan Chawe, amesema mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri miradi ya maendeleo hivyo ni muhimu kufanya tathmini ya athari za mazingira ili kukabiliana na mabadiliko hayo.

About the author

mzalendoeditor