Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya Maji Mhandisi Mbogo Futakamba akizungumza kwenye jukwaa la uhakika wa maji lililofanyika Jjijini Dodoma, lenye lengo la kujadili ufadhili wa rasilimali fedha kwa usalama wa maji ili kuboresha maisha ya wakulima wadogo na ukuaji wa uchumi wa Taifa
Wadau mbalimbali wa maji wakifuatilia kwa ukaribu jukwaa hilo.
Mwenyekiti wa mashahidi wa Maji Mhandisi Herbert Kashililah akizungumza kwenye jukwaaa la uhakika wa maji Jijini Dodoma Taifa
Mkurugenzi wa shahidi wa maji Bw.Abel Dagange akizungumza kwenye jukwaa la uhakika wa maji lililofanyika Jijini Dodoma
Wadau walioshiriki jukwaa la uhakika wa maji wakiwa katika picha ya pamoja
……………………………………………..
NA Farida Said-DODOMA
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya maji inapaswa kuchua hatua stahiki za kuweka mazingira rafiki ya matumizi sahihi ya rasilimali maji ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kuptia sekta mbalimbali zikiwemo kilimo,mifugo, viwanda na biashara.
Hayo yameelezwa kwenye jukwaa la uhakika wa maji lililofanyika Jijini Dodoma lililokuwa na ajenda kuu ya ufadhili wa rasilimali fedha kwa usalama wa maji ili kuboresha maisha ya wakulima wadogo na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Jukwaa hilo liliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la shahidi wa maji kupitia mradi wake wa utafiti wa UHAKIKA WA MAJI((Fair Water Future ) unaotekelezwa kwenye Wilaya mbili za Kilosa na Kilombero mkoani Morogoro,wenye lengo la kutambua uwajibikaji wa viongozi wa Serikali katika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji kwa shughuli za Kilimo,Mifugo na Uvuvi.
Akizungumza kwenye jukwaa hilo Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya Maji Mhandisi Mbogo Futakamba alisema kuwa bado kuna uelewa mdogo kwa wananchi juu ya mchango wa maji kwenye uchumi wa taifa hivyo kuna haja serikali kwa kushirikiana na wadau wa maji kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya maji ili kuchangia pato la nchi.
Aidha amewataka wananchi kutumia fursa zitokanzo na mabadiliko ya tabia nchi hasa katika kipindi cha mvua nyingi kwa kuhifadhi maji ili yaweze kuwasaidia kwenye shughuli mbalimbali kama Kilimo na Ufugaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mashahidi wa Maji Mhandisi Herbert Kashililah amesema kuwa lengo la jukwaa hilo ni kubadilishana uzoefu na kutoa uelewa kwa wadau wa maji kuhusu usimamizi wa rasilimali hiyo na kuweka mkakati wa namna gani wanaweza kufanya uwekeaji katika sekta ya maji kwa kutumia mifumo na fursa zilizopo.
Mhandisi Kashililah amesema kupitia tafiti walizozifanya kwenye Wilaya za Kilosa na Kilombero mkoani Morogoro wamebaini kuna mfumo unaozibana taasisi, mabonde ya maji na mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia rasilimali maji kushindwa kutekeleza na kusimamia sera na sheria zilizopo kutokana na mgawanyo wa majukumu.
Kutokana na changamoto hiyo Mhandisi Kashililah ameiomba serikali kufanya maboresho kwenye mfumo uliopo sasa ili kutoa fursa kwa Taasisi na mamlaka kufanya kazi kwa uhuru hali itakayosaidia kuweka usalama wa maji na utuzaji wa mazingira.
Tafiti zao pia zilionesha uchafuzi na uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji ambao utapelekea upungufu wa upatikanaji wa maji endelevu kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.
Naye Mkurugenzi wa uratibu wa program na usimamizi wa mazingira kutoka Wizara ya maji Mhandisi Dorisia Mulashani amesema kuwa jukwaa hilo limetoa fursa kwa wizara ya maji kushirikiana na wadau katika kupata rasilimali fedha zitakazosaidia kutunza vyanzo vya maji na kuwa na uhakika wa maji kwa taifa.
Akizungumzia mradi wa uhakika wa maji Mkurugenzi wa shahidi wa maji Bw.Abel Dagange amesema kuwa mradi huo unalenga kutoa elimu kwa wananchi ya namna wanavyoweza kujisimamia na kuwasilisha changamoto zao kwa viongozi wa serikali kwa njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari na kuandika barua kwa viongozi hao.
‘Kupitia mradi huo baadhi ya wakulima, wavuvi na wafugaji wa wilaya za Kilombero na Kilosa waliofikiwa moja kwa moja wamenufaika kwa kupata elimu iliyowasaidia kutatua changamoto zao zilizokuwa zinawakabili.”amesema Bw.Dagang.