Featured Kitaifa

PROF.KAHYARARA:’WATANZANIA MNAWEZA KUMILIKI VIWANDA VIJIJINI NA MIJINI

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara,akizungumza wakati wa kipindi cha Supa Brekfast kinachoendeshwa na Kituo cha Radio cha East Africa, jijini Dar es salaam .

………………………………..

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema Wizara imeandaa programu maalumu ya Suluhisho la Pamoja la Uwekezaji katika Viwanda inayojulikana kama “Total Industrial Solution” inayolenga kuwawezesha wananchi kumiliki viwanda kuanzia vijijini hadi mijini ndani ya miezi sita (6) kwa milioni 6 – 600.

Prof. Kahyarara ameyasema hayo Julai 7, 2022 wakati wa kipindi cha Supa Brekfast kinachoendeshwa na Kituo cha Radio cha East Africa, jijini Dar es salaam kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu programu maalumu ya Total Indusrtial Solution inayowawezesha wawekezaji wa ndani kumiliki viwanda vidogo na vya kati maeneo mbalimbali nchini.

Amesema matokeo makubwa ya programu hiyo ni kuondoa changamoto ya upungufu wa sukari na mafuta ya kula na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo ndani ya miaka miwili (2) kwa kuwawezesha wananchi kuwa na mitaji, maeneo na mashine au mitambo midogo ya kuchakata mazao hayo kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi ili kutatua changamoto mbalimbali za uhaba wa bidhaa muhimu pamoja na kuongeza ajira.

Akiongea kuhusu matokeo ya diplomasia ya uchumi, Prof. Kahyarara amesema baada ya EXPODUBAI 2020, Filamu ya Royal Tour na ziara katika nchi mbalimbali za nje, uchumi umepanda, makusanyo ya kodi kwa kila mwezi yameongezeka kutoka Tirioni 1.3 hadi Tirioni 1.9 na mauzo ya nje yameongezeka kwa asilimia 30.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepanga kutumia viwanja vya ndege vya kama lango la uchumi na kuboresha masoko ya mipakani kwa kujenga maeneo maalumu yatakayokuwa na viwanda vya uchakataji na uhifadhi wa mazao kwa ajili ya mauzo ya nje ili kurahisisha usafirishaji wa mazao hayo pamoja na kusaidia wakulima kupata soko la mazao yao kwa bei inayostahili.

Akifafanua zaidi kuhusu Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yalianza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2022.

Prof. Kahyarara amesema mwaka huu maonyesho hayo yamejumuisha makampuni yaliyoshiriki 3200 ya ndani na 180 ya nje pamoja na kongamano lilowakutanisha wawekezaji, wanunuzi na wauzaji 75 wa ndani na 21 wa nje ya nchi waliojadiliana na kuonesha uhitaji mkubwa wa mazao mbalimbali ikiwemo Mahindi na mchele kuuzwa nje ya nchi. Pia yatatambua wawekezaji walipaji kodi wakubwa watatu (3) na wanaoongoza kwa mauzo ya nje watatu (3) .

About the author

mzalendoeditor