Featured Kitaifa

WAZIRI UMMY:’MARUFUKU WAJAWAZITO KULAZIMISHWA KUCHANJA CHANJO YA UVIKO-19′

Written by mzalendoeditor

Na Zena Mohamed,Dodoma

WAZIRI wa Afya,Ummy Mwalimu amepiga marufuku wahudumu wote wa afya ambao wamekuwa wakiwalazimisha kina mama wajawazito kuchanja chanjo kwa ajili ya kinga ya virusi vya Corona na kusema suala la chanjo kwa watanzania ni hiari na sio lazima.

Ummy amesema hayo jijini hapa wakati akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao pamoja na Teddy Chaiber mwakilishi wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, ambaye ni kiongozi wa masuala ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covidi 19.

Ambapo amesema wapo Baadhi ya wahudumu wa afya ambao wamekuwa vikwazo vya huduma kwa wajawazito jambo linalopaswa kukataliwa.

“Inasikitisha sana kuona wahudumu wa afya nchini wanalazimisha kina mama wajawazito kuchanja chanjo hiyo kitu ambacho sio sawa,lazima waelewe Kuwa kuchanja ni muhimi lakini hailazimishwi,”amesema.

Aidha waziri Ummy ameongeza kuwa Tanzania ikiwa ni mwanachama wa shirika la afya ulimwenguni(WHO) na Umoja wa mataifa inaungana na mataifa yote ulimwenguni kuweza kupata kinga ya jamii dhidi ya Uviko 19 kwa angalau asilimia 70 ya watu wote duniani.

Amesema hadi kufikia jumanne tarehe 5 Tanzania imefanikiwa kuchanja watu milioni 8.5 na kuongeza kuwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Mratibu
Mkuu wa Mpango wa Utoaji Chanjo ya Uviko-19 ,Ted Chaiban, ambaye yupo nchini Tanzania kwa ziara maalumu ya siku nne,amesisitiza kwamba janga la UVIKO bado lipo na kwamba hatari ya kuibuka aina mpya ya virusi, hasa kwa makundi ambayo bado hayajapata chanjo ni kubwa.

“Janga la UVIKO-19 bado lipo kati yetu na hatuna budi kuwaambia tunawalinda wale walio hatarini zaidi, wakiwemo wazee, watu wenye maradhi sugu, watumishi wa afya walio mstari wa mbele na wale wanaofanya kazi katika sekta za utalii na hoteli,”amesema na kuongeza;

“Chanjo ndiyo kinga yetu madhubuti dhidi ya UVIKO-19 hakuna aliye salama hadi sote tuwe salama kama wanavyosema katika
Kiswahili.’Ni ujanja kuchanja”amesema

Pamoja na hayo ameeleza kuwa kabla ya mkutano na Waziri wa Afya,alifanya mkutano na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Philip Mpango ambapo kwa pamoja walijadiliana mikakati ya kuongeza kasi ya utoaji chanjo ya UVIKO-19 nchini Tanzania ili nchi ifikie malengo yake ya kuchanja wananchi.

“Ninaipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya katika kuhamasisha
chanjo dhidi ya UVIKO-19,niko hapa ili kutathmini hatua ambayo Tanzania imepiga katika kufikia malengo yake ya utoaji chanjo na kujadiliana njia za kukabiliana na vikwazo na kupanua program
ya utoaji chanjo,”amesema Chaiban.

About the author

mzalendoeditor