Featured Kitaifa

RAIS SAMIA AWAJENGEA SOKO LA KISASA WANANCHI WA PERAMIHO KUPITIA TASAF 

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akielekea kukagua ujenzi wa soko la kisasa la Peramiho linalojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.

Mwonekano wa soko la kisasa la Peramiho linalojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikagua ujenzi wa soko la kisasa la Peramiho linalojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akishuhudia shimo lililochimbwa kwa ajili ya ujenzi wa choo kitakachowahudumia watumiaji wa soko la kisasa la Peramiho linalojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Perahamiho, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.

Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Peramiho wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Neema Maghembe akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Halmashauri yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika halmashauri hiyo mkoani Ruvuma.

Mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Peramiho, akiishukuru Serikali kwa niaba ya walengwa wengine wa mpango huo na wananchi wa Peramiho, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kwa kujengewa soko la kisasa.

…………………………………

Na. James K. Mwanamyoto-Peramiho

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) anajenga soko la kisasa katika Kijiji cha Peramiho ambalo litawahudumia wananchi, kuchangia mapato na ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Mhe. Jenista amesema hayo, mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Peramiho linalojengwa na TASAF, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Ruvuma. 

Mhe. Jenista amewakumbusha wananchi wa Peramiho kuwa, wakati akiomba ridhaa ya kuwatumikia walimueleza kwamba kero yao kubwa ni kutokuwa na soko la kisasa hivyo aliwasilisha kero hiyo kwa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye aliielekeza TASAF kujenga soko la kisasa Peramiho.

“Ujenzi wa soko hili la kisasa utakamilika kwa wakati na soko hili litachangia mapato na ukuaji wa uchumi hapa Peramiho, hivyo ninaomba tulitunze kwa manufaa na maendeleo yetu,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo wa soko la kisasa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Neema Maghembe amesema kuwa ujenzi wa soko hilo ulianza rasmi tarehe 02 Machi, 2022 na mpaka sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 70.

Akizungumzia mchango wa wananchi katika ujenzi wa mradi huo wa soko, Bi. Maghembe amesema kuwa wananchi wametoa mchango wenye thamani ya shilingi milioni 3,778,000/= ambao ni sawa na asilimia 2.2 ya gharama za mradi huo na kuongeza kuwa, kazi walizofanya wananchi wa Peramiho ni kuchimba msingi, kumwagilia maji ukuta, kuchota maji na kuchimba shimo la choo.

Bi. Maghembe amesema, ujenzi wa soko hilo la kisasa unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatarajiwa kukamilika tarehe 15 agosti, 2022 kwa mujibu wa mkataba uliosaniwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara ya kikazi ya siku 3 mkoani Ruvuma iliyokuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

About the author

mzalendoeditor