Featured Kitaifa

UJENZI CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA WAFIKIA 61.4 % 

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akisaini kitabu cha wageni leo alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa chuo kipya cha ualimu cha Sumbawanga katika eneo la Pito ambapo umefikia asilimia 61 huku majengo 11 yakiwa hatua za mwisho kukamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza na watumishi wa chuo cha ualimu Sumbawanga wanaofanya kazi ya usimamizi wa mradi wa ujenzi leo alipotembelea eneo la Pito Manispaa ya Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (wa pili toka kushoto) akiwa na Mhandisi wa Ujenzi wa Mkoa huo Mhandisi Daud Sebyiga (kushoto) na Mhandisi Emanuel Didas (kulia) wakati akikagua mradi wa ujenzi wa chuo kipya cha ualimu Sumbawanga

Sehemu ya majengo mapya ya chuo cha ualimu Sumbawanga yanayoendelea kujengwa katika eneo la Pito manispaa ya Sumbawanga ambapo serikali ya Awamu ya Sita ilitoa shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa majengo 11 awamu ya kwanza .
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

…………………………………

Na. OMM Rukwa

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuwezesha upatikanaji fedha shilingi 3,852,697,911 zinazotumika katika awamu ya kwanza kujenga majengo 11 ya chuo kipya cha Ualimu Sumbawanga eneo la Pito ambapo mradi huo umefikia asilimia 61.4 hadi sasa.

Akizungumza leo (06. 07.2022) kwenye ukaguzi wa mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwaeleza waandishi wa habari kuwa serikali inatekeleza mradi huo kwa lengo la kufungua fursa za kielimu kwa wananchi ambapo utakapokamilika utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Rukwa tumenufaika na mradi huu wenye thamani ya shilingi Bilioni 3.9 ambapo majengo kadhaa yamekamilika na mengine jitihada za ukamilishaji zinaendelea vizuri. Nimeridhishwa na  kazi inayoendelea hapa na kuhusu changamoto chache nitawasiliana na Wizara ya Elimu tuzitatue mapema na mradi ufike mwisho” ,alisema Mkirikiti. 

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alipongeza Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) mkoani humo kwa kazi nzuri iliyofanya na inayoendelea kuifanya kufuatilia mwenendo wa matumizi ya fedha za umma hatua iliyosaidia mradi wa chuo hicho kutekelezwa vizuri.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Mhandisi Mshauri toka Chuo cha Ufundi Arusha Emanuel Didas alisema mradi umefikia asilimia 61.4 za ujenzi ambapo jumla ya shilingi Bilioni 2.5 kati ya shilingi Bilioni 3.0 zilizopokelewa mwezi Mei mwaka huu zimetumika hadi sasa.

Mhandisi Didas alisema jumla ya majengo 11 yamejengwa na yapo katika hatua za ukamilishaji ikiwemo jengo la madarasa lenye vyumba 8, mabweni mawili yenye uwezo wa wanafunzi 250 kila moja, vyoo vya nje, nyumba za watumishi ,jiko na bwalo na vibanda vya walinzi.

Mradi wa ujenzi wa chuo cha Ualimu Sumbawanga awamu ya kwanza kupitia mradi wa Education Program for Results (EP4R) chini ya Wizara ya Elimu ulianza 15 Agosti 2021 na unatarajia kukamilika mwaka huu. Kwa sasa chuo kinatumia majengo ya Kanisa Katoliki eneo la Kantalamba kwa ajili ya mafunzo.

About the author

mzalendoeditor