Featured Kitaifa

GRAPHITE KUANZA KUCHIMBWA RUANGWA-MAJALIWA

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia   wananchi wa kijiji cha Namikulo  akiwa katika ziara ya wilaya ya Ruangwa, Julai 5, 2022

Baadhi ya wananchi  wa kijiji cha Mihewa wakaimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowasalimia akiwa katika ziara ya wilaya ya Ruangwa, Julai 5, 2022.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari ya Matambarale wilayani Ruangwa, Julai 5, 2022. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mzee Namachi baada ya kutembelea Shule ya Msingi Chunyu wilayani Ruangwa na kuwasalimia wananchi

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Chunyu wilayani Ruangwa baada ya kutembelea Shule ya Msingi Chunyu, Julai 5, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………

*Awataka wananchi wachangamkie fursa zitokanazo na ujenzi wa mgodi huo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo katika majadiliano na kampuni ya Uranex kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa madini ya bunyu (graphite) utakaoanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wananchi wa wilaya ya Ruangwa wajiandae kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zitokanazo na ujenzi wa mgodi wa graphite.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 5, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika vijiji vya Namikulo, Namkatila na Matambarale katika kata ya Chunyu wilayani Ruangwa, Lindi.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila kwenye rasilimali kabla ya kuanza uwekezaji lazima wahusika wajadiliane na Serikali ili kubaini namna ambavyo itanufaika.”

Waziri Mkuu amesema wakazi wa maeneo hayo watakuwa ndio wanufaika wa kwanza kutokana na shughuli mbalimbali zinakazokuwa zikiendelea kuanzia hatua ya ujenzi hadi uzalishaji.

“Kila shughuli itakayofanyika hapa ni fursa kwetu sisi wana-Namikulo na wana-Ruangwa kiujumla. Tujipange sawa sawa Serikali yenu ipo makini kuhakikisha mnanufaika na mradi huo.”

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kampuni ya Uranex, Mhandisi Isaac Mamboleo amesema kampuni yao inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi huo katika mwaka huu wa fedha.

Amesema mradi huo ambao utahusisha vijiji saba unatarajia kugharimu shilingi bilioni 625 na utazalisha ajira 950 kati yake ajira 600 wakati wa ujenzi na ajira 350 wakati wa uzalishaji.

Mhandisi Mamboleo amesema kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 59 zenye gharama ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuwafidia baadhi ya wananchi waliopisha ujenzi wa mradi huo.

Amesema baada ya kukamilisha ulipaji fedha kama fidia ya ardhi na mazao, pia wanajenga nyumba zenye ubora kwa ajili ya kuwafidia wananchi 59 waliokuwa na nyumba katika eneo la mradi. “Nyumba hizo tunajenga nje ya eneo la mradi na kila mtu anajengewa nyumba kulingana na ukubwa wa nyumba yake ya awali.”

Nao, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wameziomba kampuni za uwekezaji zitoe kipaumbele kwa wananchi wanaoishi karibu maeneo ya mradi na kwamba wamejipanga na wako tayari kwa kazi

About the author

mzalendoeditor