Featured Kitaifa

TAASISI YA IPRT,CHUO CHA DAYSTAR CHA KENYA ZAINGIA MAKUBALIANO KUWANOA WADAU WA MAWASILIANO YA UMMA

Written by mzalendoeditor

Mratibu Mafunzo wa Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania IPRT Dk. Titus Simsamba (kulia) pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo cha Daystar Prof. Laban  Ayiro (kushoto) wakipongezana mara baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji (MOU) baina ya taasisi hizo ili kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika hapa nchini. Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika jijini Dar es Salaam 

Mratibu Mafunzo wa Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania IPRT Dk. Titus Simsamba (kulia) pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo cha Daystar Prof. Laban  Ayiro (kushoto) wakisaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji (MOU) baina ya taasisi hizo ili kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika hapa nchini. Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika jijini Dar es Salaam

Makamu Mkuu wa Chuo cha Daystar cha nchini Kenya  Prof. Laban  Ayiro (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji (MOU) baina ya chuo hicho na Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma Tanzania (IPRT) ili kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika hapa nchini. Kulia ni Mratibu Mafunzo IPRT Dk. Titus Simsamba. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam

………………………………….

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam:

Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT) imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji (MOU) baina yake na Chuo Kikuu cha Daystar cha nchini Kenya.

Kupitia makubaliano hayo taasisi hizo mbili zitashirikiana kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati (strategic communication and leadership) mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika hapa nchini.

Makubaliano hayo yalisainiwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo ilishuhudiwa Mratibu wa mafunzo Taasisi ya IPRT Dk. Titus Simsamba pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo cha Daystar Prof. Laban  Ayiro wakiwakilisha taasisi hizo mbili katika utiaji saini makubaliano hayo yanayoashiria mwanzo wa safari ya pamoja katika kutimiza adhima hiyo muhimu.

“Lengo moja kuu la makubaliano haya yanayoshuhudiwa hii leo ni kuongeza ufanisi katika mafunzo tunayoyatoa kwa walengwa wa kozi zetu’’ alisema Dk Simsamba kwenye hafla hiyo iliyohudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo wakufunzi kutoka Chuo cha Daystar pamoja na wenzao kutoka hapa nchini.

Dk Simsamba alibainisha zaidi kuwa kupitia makubaliano hayo wadau mbalimbali wa mawasiliano na uongozi hapa nchini wakiwemo waandishi wa habari watakuwa kwenye nafasi ya kushiriki mafunzo mbalimbali ya kujinoa kitaaluma yatakayotolewa na wataalamu kutoka chuo cha Daystar pamoja na wataalam wa ndani kupitia taasisi ya IPRT.

“Habari njema ni kwamba hatua hii muhimu inakuja ikiwa ni siku chache tu tumetoka kukamilisha mafunzo ya kwanza kabisa kupitia programu hii tuliyoyafanya ndani ya wiki moja huko mkoani morogoro ambapo walengwa walipata wasaa kujifunza kozi mbalimbali ikiwemo mawasiliano ya kimkakati kwa taasisi na mashirika, mawasiliano wakati wa mgogoro (crisis communication), usimamizi wa chapa (brand management), mawasiliano fanisi, mawasiliano binafsi na mawasiliano ya kitaasisi,’’

“Mafunzo hayo hayakuishia darasani tu bali pia washiriki walipata wasaa wa kutembelea Hifadhi ya  Taifa ya Mikumi iliyopo mkoani Morogoro ambapo walipata  fursa ya kufurahisha nafsi zao kwa kutazama vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo sambamba na kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassani kwa kutangaza utalii wa ndani,’’ alisema

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Daystar Prof. Laban  Ayiro alisema makubaliano hayo baina ya taasisi  hizo mbili zinazotoka kwenye mataifa mawili yanayounda Jumuiya moja ya Afrika Mashariki ni muendelezo wa mahusiano imara baina ya wananchi na serikali zinazounda Jumuiya hiyo hususani katika nyanja nzima ya kitaaluma kupitia mawasiliano ya Umma na uongozi,

“Kwetu sisi huu umekuwa ni mwanzo mzuri sana kwa kuwa si tu tutakuwa tunakuja kutoa mafunzo bali pia na sisi tutapata nafasi ya kujifunza zaidi kutoka kwa wenzetu wa Tanzania kwa kuwa mafunzo tunayoyatoa ni ya kiutendaji zaidi na hivyo yamekuwa yakihusisha mijadala ambayo mwisho wa siku inatujenga wote. Lengo kubwa ni kuhakikisha washiriki wa mafunzo haya wanapata kile walichotarajia kukipata baada ya kukamilika kwa mafunzo,’’ alisema.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo mpya baina ya taasisi yake na IPRT utatekelezwa kwa urahisi zaidi kwa kuwa taasisi zote mbili zina nia ya pamoja ambayo ni kutoa mafunzo kwa wanataaluma wa mawasiliano ya umma na uongozi ili kuwawezesha kutekeleza wito wao wa utoaji huduma kwa kuzingatia weledi, ubunifu na ujuzi unaotakiwa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Morogoro, Padre Masoke Edward alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa yamewajenga zaidi washiriki wakiwemo viongozi wa dini ambao wanakutana na kuwasiliana na makundi ya watu mbalimbali, hivyo mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwao.

About the author

mzalendoeditor