Featured Kitaifa

KAMPENI YA UCHANGIAJI DAMU SALAMA YA ‘MC MZUNGU MWEUSI’ YALETA MATOKEO CHANYA

Written by mzalendoeditor


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
 
Mratibu wa Kampeni ya Uhamasishaji wa kuchangia damu kwa hiari Amos John maarufu MC MZUNGU MWEUSI amewashukuru wananchi walioshiriki kampeni hiyo iliyokwenda sanjari na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23,2022 huku akiiomba jamii kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine.

Ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 2,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya wananchi kushiriki zoezi la kuchangia damu kwa hiari ambalo limefanyika kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
 
Amos John ambaye ni Mwandishi wa Habari na mtangazaji wa Radio Kwizera Fm mkoa wa Shinyanga amewasisitiza wananchi kuendelea kuunga mkono shughuli za uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wakiwemo wajawazito, watoto na wahanga wa ajali.
 
Amesema aliguswa na kuamua kuandaa Kampeni ya damu salama kwa lengo la kuhamasisha jamii kujenga utaratibu wa kuchangia damu ambapo ameshirikiana na kitengo cha damu salama Manispaa ya Shinyanga.
 
”Niliguswa na kuamua kushirikiana na kitengo cha damu salama Manispaa ya Shinyanga kuandaa kampeni ya damu salama kwa lengo moja tu la kuhakikisha tunahamasisha wananchi kujenga utamaduni kuchangia damu ili waweze kuokoa maisha ya ndugu zetu wenye uhitaji wa damu”,amesema Amos.
 
Naye mratibu wa huduma za maabara Manispaa ya Shinyanga Saumu Ibrahim amesema Kampeni hiyo imekuwa na mafanikio kwani wananchi wamejitokeza kuchangia damu.
 
“Tunamshukuru Mungu kwa leo tumeweza kupata UNIT zaidi ya 14 na mahitaji yetu kwa Manispaa kwa siku tunahitaji kutumia UNIT 9 tunaimani kwamba tumepata kitu cha kuweza kuwasaidia watu wenye uhitaji, wito wangu kwa wananchi wa Shinyanga wajitokeze kuchangia damu. 
 
Suala la damu kila mtu ni mhitaji wa damu mtarajiwa ukipata mgonjwa mwenye shida ya damu au ukipata shida ya damu ndiyo utajua umuhimu wa kuchangia damu na suala la damu limekuwa ni changamoto mno kwahiyo uhitaji wa damu ni mkubwa niwaombe sana watanzania kwa ujumla tuguswe kwa kuona umuhimu wa kuchangia damu”, amesema Saumu.
 
Baadhi ya Wakazi mkoani Shinyanga ambao wameshiriki zoezi kampeni hiyo wameeleza kuwa wamehamasika katika zoezi la uchangiaji damu kwa lengo la kusaidia watu wenye uhitaji huku wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa ajili ya kuchangia damu ili kuwasaidia wahitaji.
 
Aidha wananchi hao wamewashukuru waandaaji wa kampeni hiyo ya kuchangia damu ambapo wamesema itasaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa damu salama.
MC Mzungu Mweusi  akielezea kuhusu Kampeni ya Uchangiaji damu salama


Wananchi wakiendelea kuchangia damu


 
 

About the author

mzalendoeditor