Featured Kitaifa

‘WANAWAKE TUMIENI VYAKULA VYENYE MADINI YA FOLIC ILI KUZUIA KUZAA WATOTO WENYE TATIZO LA KICHWA KIKUBWA NA MGONGO WAZI’: WAZIRI UMMY

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza baada ya kushiriki kwenye mbio za marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu kwa Watoto 200 wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi zilizofanyika Jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akitoa vyeti kwa washiriki  baada ya kushiriki kwenye mbio za marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu kwa Watoto 200 wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi zilizofanyika Jijini Dar Es Salaam.

 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akishiriki mazoezi pamoja na watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa wakati aliposhiriki  kwenye mbio za marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu kwa Watoto 200 wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi zilizofanyika Jijini Dar Es Salaam.

…………………………………………

Na WAF, Dar ES Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa wito kwa wanawake walio kwenye umri wa kuzaa au wanaopanga kupata watoto kula vyakula vyenye kuongeza madini ya ‘Folic’ ili kuongeza kinga ya kumkinga mtoto dhidi kuzaliwa na changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa.

Waziri Ummy amesema hayo leo mara baada ya kushiriki kwenye mbio za marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu kwa Watoto 200 wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi zilizofanyika Jijini Dar Es Salaam.

“Tatizo la Watoto kuzaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi tunaweza kulizua, linatokana na ukosefu wa ‘Folic Acid’, sasa wanawake walio kwenye umri wa kuzaa na walio katika mipango ya kupata Watoto waanze kutumia vyakula ambavyo vitawapa madini ya fluoric” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa watoto wanaozaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi bado ni tatizo hapa nchini huku takwimu zinaonyesha katika nchi tano barani afrika zenye Watoto wengi wanaozaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi, Tanzania tuko namba tatu tukitanguliwa na Algelia na Ethiopia.
Waziri Ummy amesema kwa hapa nchini katika kila Watoto 1000, Watoto 3 wanazaliwa na tatizo la mgongo wazi na kichwa kikubwa huku akisema kuwa takwimu za Watoto wanaozaliwa kila mwaka hufikia takribani milioni 2, hivyo Watoto 6000 kila mwaka huzaliwa na matatizo hayo.

“Lengo letu ni kuzuia watoto wenye matatizo haya wasizaliwe hapa nchini, kwa hiyo tutaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za uzazi hususani kabla ya kujifungua, wakati wa ujauzito na kujifungua” amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu

Aidha,Waziri Ummy amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha madini ya fluoric yanapatika kwa urahisi katika ngazi zote za kutolea huduma za afyahadi ngazi ya Zahanati.

Hata hivyo Waziri Ummy amewataka Madaktari, Wakunga na Wauguzi pindi wanapozalisha na kuona mtoto mwenye dalili za kichwa kikubwa na mgongo wazi watoe rufaa ili Watoto waweze kupata huduma mapema.

Katika kutilia mkazo kuwahi kwa upatikanaji wa matibabu Waziri Ummy ametoa wito kwa wazazi na walezi kutowaficha Watoto wanaozaliwa na tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi wawapeleke kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kufanyiwa upasuaji na kuendelea na maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Taasisi ya Mifupa MOI Prof. Charles Mkony amemshukuru Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kushiriki mbio hizo na kuendelea kuiunga mkono Taasisi ya Mifupa MOI kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Prof. Mkony amesema Taasisi ya MOI imekuwa ikitoa huduma za matibabu kwa Watoto wenye matatizo hayo huku akiuomba umma wa Watanzania, Mashirika na watu binafsi wenye uwezo wa kiuchumi kuchangia katika matibabu ya Watoto hao ambao hawana uwezo wa kujilipia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema kupitia fedha walizoweza kuchangisha tayari wameweka kambi ya kuanza kutoa huduma za matibabu huku Watoto 20 tayari wakiwa wameshapata matibabu.

About the author

mzalendoeditor