Featured Kitaifa

BASHUNGWA ATANGAZA WAOMBAJI WALIOKIDHI VIGEZO NA KUPANGIWA VITUO KADA YA AFYA NA WALIMU

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu ajira hizo zilizotangazwa Aprili, Mwaka huu

……………………………………

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imetangaza waombaji waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo katika kada ya Afya na Walimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26,2022 wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu ajira hizo zilizotangazwa Aprili, Mwaka huu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa.

Waziri Bashungwa,amesema kwa upande wa kada za Afya, Waombaji wenye sifa waliokidhi  vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia  53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61 

Aidha kutokana na  uchache wa waombaji wenye sifa wa kundi hilo nafasi 736 kada za Afya zilikosa waombaji wenye sifa.

‘’ Kada hizo ni Daktari wa Meno 50, Tabibu Meno 43, Tabibu  Msaidizi 244, Mteknolojia Mionzi 86 na Muuguzi- ngazi ya  cheti 313. Kada hizi zitarudiwa kutangazwa ili kupata waombaji  wenye sifa watakaojaza nafasi hizo’’amesema Waziri Bashungwa

Kwa upande wa kada za Ualimu, Waziri Bashungwa amesema kuwa waombaji wenye sifa waliokidhi  vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo jumla ya  walimu 5,000 wamepangwa shule za Msingi na walimu 4,800 Shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu wa shule  za Msingi na Sekondari 261. 

Amesema kuwa Kati ya Walimu 5,000 wa shule za Msingi wanawake ni 2,353  sawa na asilimia 47.06 na wanaume ni 2,647 sawa na asilimia  52.94,Kwa upande wa walimu 4,800 wa Shule za sekondari wanawake ni 1,289 sawa na asilimia 26.85 na wanaume ni  3,511 sawa na asilimia 73.15.

‘Walimu wenye ulemavu  261 wa shule za Msingi na Sekondari walioajiliwa ni sawa na  asilimia 2.66 ya walimu wote walioajiliwa wakiwemo wanawake  84 na wanaume 177. Napenda ieleweke pia kuwa, kwa walimu  wa sekondari tumetoa ajira za walimu wa sayansi kwa asilimia  76 ya nafasi 4,800 tulizopewa.”amesema

Waziri Bashungwa amesema kuwa hadi kufikia Mei 8, Mwaka huu maombi 165,948 yakiwamo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya kada za afya  ni 42,558, na ualimu ni 123,390.

“Ili kufanikisha mchakato wa ajira, Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliunda Timu Maalum, ya kufanya uchambuzi wa maombi ya ajira, iliyohusisha taasisi mbalimbali,”amesema.

Bashungwa amezitaja  taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Zingine ni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (NACTVET), Sekretarieti ya Ajira, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Mabaraza ya Kitaalamu katika Sekta ya Afya.

Aidha Waziri Bashungwa amewaagiza waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14, kuanzia leo watakuwa wamepoteza nafasi zao na zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa,waliopo kwenye Kanzidata ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

“Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo Waajiriwa wapya wamepangwa, wawapokee na kuwawezesha kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma, na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwao,”amesema.

Hata hivyo amefafanua kuwa taarifa za kuripoti waajiriwa hao zijazwe kwenye mfumo wa kielektroniki (ajira.tamisemi.go.tz), baada ya kila mtumishi kupokelewa na kukamilisha taratibu.

About the author

mzalendoeditor