Featured Kitaifa

WALIOHUSIKA NA MAUAJI YA PADRE JIJINI MBEYA WASAKWA NA POLISI

Written by mzalendoeditor

Mnamo tarehe 11.06.2022 majira ya saa 05:00 asubuhi huko maeneo ya Sabasaba katika Mto Meta, chini ya Daraja la Jakalanda, Kata na Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya. Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya MICHAEL MAWELERA SAMSON [63] Raia wa Malawi ambaye alikuwa akihudumu katika shirika la Missionaries of African (WHITE FATHERS) alikutwa akiwa ameuawa na mwili wake ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili na kisha kuviringishwa kwenye Duveti (Matress) na Blanket na kutupwa kwenye mto huo na mtu/watu wasiofahamika. 

Chanzo cha tukio hili kinachunguzwa.  Awali mnamo tarehe 10.06.2022 majira ya saa 11:00 jioni Padre huyo aliwaaga wenzake kuwa anakwenda kufanya mazoezi ya kutembea na hakurudi tena mpaka alipokutwa akiwa ameuawa umbali wa takribani kilomita 2 kutoka maeneo ya Parokiani (YOUTH CENTER) wanapoishi na mapadre wenzake wa shirika hilo. Msako unaendelea kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.   

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linalaani vikali tukio hili baya kutokea ndani ya mkoa wetu kwa siku za hivi karibuni. Aidha tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mtu/watu waliohusika na tukio hili kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili watuhumiwa wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Pia Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na upelelezi wa tukio hili ili kubaini chanzo chake na waliohusika kwa hatua zaidi za kisheria.

About the author

mzalendoeditor