Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na Wananchi pamoja na Wafanyakazi wa Kiwanda cha Kagera Sugar mara baada ya kuzungumza nao
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wananchi wa Bukoba mjini alipowasili katika Uwanja wa Kaitaba kwa ajili ya kuhutubia Mkutano
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Wananchi wa Bukoba mjini katika Mkutano wa Hadhara katika Uwanja wa Kaitaba mkoni Kagera
…………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Kagera una fursa kubwa ya kiuchumi na kibiashara, hivyo unapaswa kupewa kipaumbele katika mipango na mikakati ya maendeleo.
Rais Samia amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Aidha, Rais Samia amesema, Mkoa wa Kagera ni wa kimkakati katika kuinua uchumi wa nchi kwa kuwa unapakana na nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa onyo kwa Vyama vya Ushirika kuacha kunyonya wakulima wa kahawa mkoani humo na kuwaacha wauze mazao yao kulingana na bei wanayoitaka.
Rais Samia pia, amesema bei ya mauzo ya kahawa haipaswi kuwa na makato kwa kuwa Serikali inatoa ruzuku katika pembejeo.
Halikadhalika, Rais Samia amewataka Waziri wa Ardhi pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kushughulikia changamoto ya uhaba wa malisho na uwepo wa migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo mkoani humo.
Kuhusu uvuvi, Rais Samia amesema Serikali inafanya jitihada ya kuinua sekta ya hiyo ikiwemo kununua boti na kuongeza fedha kwenye mfuko wa uvuvi kwa wavuvi wadogo ili kuwakomboa kuwainua kiuchumi.