Featured Kitaifa

MIKAKATI YA SERIKALI KWENYE KITUO CHA TUNDUMA

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango,Hamad Hassan Chande amesema katika kurahishisha biashara kati ya nchi ya Tanzania na Zambia na kuondoa tatizo la msongamano wa magari katika Kituo cha Tunduma, Serikali inaendelea kuchambua na kutathmini taratibu zilizopo ili kuona kama kuna uwezekano wa kuongeza Kituo cha Forodha.

Hatua hiyo ni miongoni mwa hatua nne zilizochukuliwa na Tanzania na Zambia katika kuondokana na tatizo la msongamano wa magari kituo cha Tunduma.

Naibu Waziri Chande amesema hayo Juni 8,2022,bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichwale.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji ni lini serikali itaongeza geti jingine ndani ya Jimbo la Momba kutokana na geti la Tunduma kuzidiwa katika kutoa huduma.

Chande amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuondokana na tatizo hilo ambapo Januari 2021 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliingia makubaliano na Mamlaka ya Mapato Zambia yanayoelekeza hatua mbalimbali za kuchukua kwa kila nchi.

Ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuunganisha mfumo wa TANCIS wa TRA na mfumo wa ASCUDA World wa Zambia ili kuiwezesha Idara ya Forodha Zambia kupata taarifa za shehena ya mzigo husika kabla kuwasili mpakani.

“Serikali ya Zambia imefanya maboresho ya miundombinu ya barabara na eneo la kuegesha magari kupitia ufadhili wa TMEA (Trademark East Africa),na kwa upande wa Tanzania imeanzisha Kituo cha Pamoja cha Forodha (One Stop Border Post, OSBP) ambacho kimesaidia taasisi zote za Serikali kuwa sehemu moja na kuwasiliana kwa haraka,”

“Pia kupitia ufadhili wa TMEA serikali imenunua scanners tatu ambazo ni baggage scanner na body scanner ambazo zinafanya kazi na cargo scanner inayotarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi Julai 2022,”amesema.

About the author

mzalendoeditor