Featured Kitaifa

CWT KWA KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LA FES PAMOJA NA WADAU WA ELIMU WATOA MAPENDEKEZO KUHUSU ELIMU

Written by mzalendoeditor

 Mkuu wa Idara ya elimu kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Stella  Kiyabo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na  Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES) jijini Dodoma.

Muwakilishi wa Friedrich Ebert Stiftung (FES) Bi. Anna Mbise ambaye pia ni Afisa Miradi,akielezea jinsi wanavyosaidiana na wadau wa maendeleo ya elimu katika mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na  Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES) jijini Dodoma.

Mwalimu Mwandamiza wa Taaluma kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Kowak,Mwl Gerald Orembe,akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na  Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES) jijini Dodoma.

Mwakilishi wa walimu wananwake CWT Tanzania Mwl.Elizabeth Werema,akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na  Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES) jijini Dodoma.

 SEHEMU ya Washiriki wakifatilia Hituba ya Mkuu wa Idara ya elimu kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Stella  Kiyabo (hayupo pichani) wakati katika mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na  Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES) jijini Dodoma.

………………………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

WADAU wa elimu wakiongozwa  na Chama cha Walimu Tanzania (CWT)  wamependekeza  mambo kadhaa ikiwemo kukomesha vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwani imebainika kuwa maadili yameshuka katika shule  na jamii kwa ujumla.

Akiyataja mapendekezo hayo mbele ya Waandishi wa Habari jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na  Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES) Mkuu wa Idara ya elimu kutoka CWT, Stella  Kiyabo amesema imebainika kuwa maadili yameshuka katika shule  na jamii kwa ujumla na  vitendo vya kikatili dhidi ya watoto /wanafunzi vimezidi na hivi havikubaliki.

Pia,amesema  wanapendekeza kuzingatiwe  ajira kwa Walimu Wenye Taaluma kwani   ualimu ni taaluma hivyo  serikali ihakikishe kama ilivyo kwa shule za umma, shule zote za binafsi zinaajiri walimu wenye Taaluma ya Ualimu kufundisha shule za binafsi kama taratibu katika usajili wa shule zinavyoelekeza.

“Kuzingatia Mikataba na Maslahi (Compliance to Contract as a Legal requirement): Kwa kutambua umuhimu wa mkataba wa ajira kama ilivyo kisheria, Walimu wa Shule Binafsi wapatiwe mikataba ili kuwahakikishia usalama wa ajira zao na kama sehemu ya kuheshimu taaluma yao na utendaji kazi wao,“amesema

Vilevile, Maslahi ya Walimu yazingatie kima cha chini cha mshahara kinachopendekezwa na serikali na maslahi mengineyo ili kuhakikisha wanaweza kujikimu na kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Kwa kuwa makazi ni sharti muhimu la kimaslahi ya walimu kuweza kuishi katika mazingira mazuri, nadhifu, yenye kufikika na yenye hadhi na staha, Mwongozo wa Usajili wa shule wa mwaka 2020 ufanyiwe mapitio na kuweka bayana kuwa Uhakika wa Makazi Bora ya Walimu wa Umma na Binafsi viwe  vigezo muhimu vya shule kupatiwa usajili, na ubainishe nani anahusika na suala la makazi ya Walimu,“amesema

Pia,kwa kujua kuwa serikali imeandaa shule za Mfano, iweke sharti la shule zingine za umma na za binafsi kukidhi vigezo muhimu vilivyobainishwa katika shule za mfano ili ziwe kielelezo kwa shule za binafsi.

“Hii itapelekea shule za umma  kukidhi huduma bora za utoaji wa Elimu ambazo wachache hulazimika kuzitafuta katika shule binafsi. Shule za umma ziwe mfano kwa mazingira yake, maslahi kwa walimu wake, miundombinu na uzingatiaji wa vigezo,“amesema.
Amesema kufuatia vuguvugu la mjadala wa mabadiliko ya Sera na Mitaala ya Elimu, utoaji wa Elimu kupitia sekta binafsi uzingatie,  haki ya mtoto kupata elimu bila kubugudhiwa,haki ya maslahi na Mikataba yenye kuzingatia matakwa ya sheria kwa walimu.

Vilevile,kuajiri walimu wenye taaluma ya Ualimu ili kuhakikisha elimu itolewayo ni bora na yenye kuwajenga wanafunzi  na ujumuishi kwa walimu na Wanafunzi wenye ulemavu.

“Serikali ihakikishe kuwa inaweka sheria kuhakikisha shule binafsi zinaweka mazingira wezeshi kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu wanapata elimu kama wenzao wasio na ulemavu.
Pia,Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule za umma ili iweze kuwa rafiki kwa watoto wenye ulemavu. Alisema kuwa kuboresha elimu Tanzania kutasaidiwa Zaidi na kuwepo na mipango thabiti ya ukusanyaji wa kodi na matumizi sahihi ambapo walimu, wamiliki wa shule na wanajamii wamekuwa wakilipa kodi.

Mianya ya upotevu wa mapato izibwe pia kuhakikisha fedha za umma zinafanya kazi ya kuboresha huduma za kijamii na si kufaidisha wachache. 

MAMBO YA KUFANYA

Mkuu wa Idara ya elimu kutoka CWT,amesema kama taifa wameweza  kushuhudia mafanikio mengi katika sekta ya elimu.
Amesema Mafanikio hayo yamechochewa na msukumo wa serikali katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa mojawapo ya sekta za vipaumbele.
Mafanikio hayo yametokana pamoja na mambo mengine, uwezo wa Taifa na Viongozi wake pamoja na kuhakikisha wanaweka msukumo katika kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu;
Kuhakikisha kuna miundombinu yenye kuwezesha upatikanaji wa elimu.Kuajiri walimu na wataalamu wa masomo husika ambao hulipwa na serikali,Kuandaa sheria, sera, mitaala na nyaraka zenye kuongeza msukumo wa kufikia lengo la Taifa la kuwapatia wananchi wake Elimu.
“Kufanya mabadiliko ya sera na mitaala ili kuendana na mabadiliko ya mipango ya maendeleo ya Taif ana dunia kwa ujumla,”amesema

MABORESHO MAKUBWA YA SIKU ZA USONI

Amesema yapo mabadiliko ya sekta ya elimu kwa siku za usoni ambayo kama wadau hatuna budi kuipongeza serikali na Wizara husika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Madarasa kwa shule za Msingi na Sekondari.
Pia,kurejeshwa kwa Watoto wakike walioacha shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo mimba.
“Nia ya kutaka kufanya mapitio na kisha kuboresha Sera ya Elimu na Mitaala ili kukidhi mahitaji ya wakati,Kutangazwa kwa nafasi za ajira, ambapo walimu wengi wataajiriwa kupunguza uhaba mkubwa  ambao umekuwepo kwa muda mrefu
“Kutoa kipaumbele kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi, kwa kuanzisha shule ya sayansi na ya bweni kwa mikoa yote 26 ya Tanzania bara,”amesema.

SEKTA BINAFSI
Amesema ushiriki wa sekta binafsi katika kutoa elimu umeongezeka, ambapo ongezeka kubwa la idadi ya shule za binafsi (8% ya shule zote za msingi na 25% ya shule zote za Sekondari.
Amesema idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata elimu katika shule binafsi (4% wanafunzi wote wa shule ya msingi wakiwa Shule binafsi)
“Kutoa nafasi za ajira kwa Walimu na Wafanyakazi wengine kupitia shule na taasisi za elimu binafsi,Kuongeza chachu ya ushindani na matokeo katika mitihani ya Taifa,Kuongezeka kwa Watoto wa Kike wanaofanya vizuri katika mitihani ya Taifa.

CHANGAMOTO
Amesema pamoja na matokeo  chanya, pia yapo matokeo hasi yanayoikabili sekta ya elimu kama  uhaba wa miundo mbinu katika shule za umma na za binafsi.
“Uhaba  wa Walimu katika shule za umma na za binafsi,Usimamizi usio imara wa shule mfano, Kuajiri watu wasio na taaluma ya ualimu kufundisha shule hususani kwa shule binafsi kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji.

“Baadhi ya walimu kulipwa mshahara mdogo usiokidhi viwango vinavyopendekezwa hasa kwa baadhi ya shule binafsi, Kutoweka msisitizo wa Makazi ya walimu kama kigezo muhimu kabla ya shule kusajiliwa na hivyo kupelekea walimu wengi kupata adha ya makazi hasa Wanawake,“amesema.

Pia,sera ya elimu iliyoruhusu ubinafsishaji wa elimu haijaweka bayana utoaji wa elimu kwa kuzingatia mahitaji ya Jinsia na Ujumuishi kwa Walimu na Wanafunzi hasa upatikanaji wa huduma za msingi

JINSI YA KUONDOA CHANGAMOTO
Amesema Serikali ikusanye kodi inavyostahili, tafiti mbalimbali zinaaonesha kuwa wigo wa walipa kodi ni mdogo sana hapa nchini, watu wengi waliopo kwenye sekta isiyo rasmi hawalipi kodi (ripoti ya utafiti ya ActionAid 2021).
“Kutokusanya mapato ya kutosha hupelekea serikali kuwa na uwezo mdogo wa kugharamia huduma za msingi kama elimu, ikiwa ni pamoja na kutowapandisha walimu madaraja, kushindwa kutoa posho za likizo kwa walimu, na hata mafao ya kustaafu,”amesema.
Vilevile serikali izibe mianya yote ambayo inasababisha upotevu wa mapato.
“Utafiti wa ActionAid wa 2021 ulionesha kuwa serikali inapoteza takribani 17.4 Trilioni kila mwaka, kuanzia 2013, fedha hizi ni nyingi sana na zingeweza kugharamia vizuri kabisa utoaji wa huduma za msingi za jamii kama elimu, afya, maji, ulinzi nk na shughuli nyinginezo za maendeleo,”amesema.

Serikali isimamie kikamilifu rasilimali tulizo nazo kwani kumekuwepo na upotevu wa fedha za umma kama unavyobainishwa na ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali.
“Hizi ni fedha za umma, fedha za walipakodi na wavuja jasho, ambazo zilipaswa kutoa huduma za jamii kama elimu, afya, maji nk. Kama chama cha wafanyakazi/asasi za kiraia, tunakemea kwa nguvu zote ubadhirifu wa kila namna.

Kwa upande wake Muwakilishi wa Friedrich Ebert Stiftung (FES) Bi. Anna Mbise (Afisa Miradi) amesema kuwa shirika lake limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali vyama vya wafanyakazi wakiwa miongoni katika kutekeleza miradi ya kukuza usawa, demokrasia na haki za wafanyakazi na jamii kwa ujumla.

Amesema kuwa itakuwa vema kama serikali itaendelea kuweka kapaumbele cha juu katika kusimamia elimu katika shule za umma na za binafsi na kuhakikisha kuwa watoto wanasoma katika shule zenye ubora, miundo mbinu ya kutosha na jumuishi kiasi kwamba mtoto wa kitanzania hataamua kusoma shule binafsi kwa sababu shule za umma hazina ubora.

Hayo yote yanawezekana kama serikali itaweza kukusanya kodi vizuri na kuzielekeza katika kuboresha huduma za jamii Pamoja na ushirikiano mzuri kati ya serikali na wadau wengine.

About the author

mzalendoeditor