Featured Michezo

SERENGETI GIRLS YAFUZU KOMBE LA DUNIA NCHINI INDIA

Written by mzalendoeditor

Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’ imefuzu kucheza Kombe la Dunia nchini India, Oktoba mwaka huu baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-1.

Serengeti ilipata ushindi wa bao 1-0 jana, lililowekwa kimiani na Neema Paul kwa kichwa dakika ya 50 akiunganisha mpira wa kona uliochongwa na Veronica Mapunda, huku katika mechi ya awali iliyopigwa Cameroon, timu hiyo ilishinda mabao 4-1.

Tanzania sasa imeungana na Morocco na Nigeria kuiwakilisha Afrika na kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazoshiriki fainali hizo za Dunia zitakazopigwa kati ya Oktoba 11-30 katika miji mitatu nchini India zikiwa fainali za saba tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 2008.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu fainali hizo kwa timu za soka na hadi kupenya kwenye kwenda India, Serengeti ilizing’oa Botswana kwa jumla ya maba0 11-2, kisha Burundi na kumalizana na Cameroon jana ambao waliugomea mchezo huo kwa saa zima kupiga wachezaji wao watatu kuzuiwa kucheza kwa madai ya kukutwa na Uviko-19.

Hata hivyo, timu hiyo ililazimika kurudi uwanjani baada ya majadiliano ya muda mrefu na kamisaa na maofisa wa mchezo huo na ndipo dakika 45 zikaisha bila bao kabla ya Serengeti kurudi na moto na kuwakimbiza wageni wao na kupata ushindi huo.

Hata hivyo, kinara wa mabao wa mashindano hayo kwa hatua hii ya mchujo akifunga 10, Clara Luvanga alilimwa kadi nyekundu dakika za majeruhi.

About the author

mzalendoeditor