Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU AICHAMBUA SEKTA YA UTALII

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wa kuitangaza Programu ya Tanzania The Royal tour na kusema yoyote anayebeza kazi iliyoifanyika hajui maana ya utalii.

Kutokana na hilo amewashauri watanzania na wizara ya Maliasili na Utalii kumuunga mkono kwa kuendelea kuitangaza vizuri kazi hiyo na sio kuiacha ipotee.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Juni 3,2022,Jijini Dodoma Mtaturu amesema Rais ametutoa kimasomaso kuitangaza nchi kiutalii.

“Rais Samia amefanya kazi nzuri na sisi tunaona ina maana kubwa sana kama nchi,imeenda kuzinduliwa katika sehemu ambayo watu hawavijui vivutio vyetu,imeenda kuzinduliwa katika nchi za Ulaya,nina amini kabisa wale walioshiriki kuona vivutio vile leo tunaona matokeo yake,sasa yule ambaye anaenda kubeza au kukosoa hajui maana ya utalii tumuache ,

“Kuna nchi zimefanya kazi kubwa ya kutangaza vivutio vyao, sisi tumefanya kwa kiasi, lakini mkuu wan chi alivyoingia na kufanya jambo hili limetupa heshima kubwa duniani ,na leo hii ile film kila mtu akiangalia anajua kabisa anatoka Ulaya anakwenda kuona Serengeti,mlima Kilimanjaro anaenda kuona vivutio vya kipekee ambavyo ni vya kipekee katika nchi yetu,”ameongeza.

Ametoa rai kwa watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais na wizara iendelee kuitangaza vizuri kazi hiyo na kutokubali ipotee.

“Kazi hii ni kubwa na ina heshima,kiongozi wa nchi kuacha kazi zake na kuingia kufanya kazi ya sekta ni jambo kubwa na la kutiwa mfano ,na matokeo tumeanza kuyaona watu wanakuja nchini kwetu kwa ajili ya kuona vivutio vyetu,”ameongeza.

Mtaturu amempongeza pia waziri wa Maliasili na Utalii Pindi Chana kwa kupewa heshima kubwa ya kuongoza sekta hiyo na kusema wanamjua kuwa ni mtu anayejua namna ya kufanya kazi na alishafanya vizuri kwenye eneo la diplomasia.

“Sisi tuna Imani na wewe,na tunajua kwa kushirikiana na Naibu Waziri,katibu Mkuu na viongozi wengine mtafanya vizuri,na sisi tutaendelea kuwaunga mkono ili lengo la nchi la kufikisha watalii milioni 5 kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inavyosema liweze kufikiwa,”amesema.

USHAURI KWA WIZARA.

Mtaturu ameishauri wizara mambo manne ikiwemo kuwa na dirisha moja la ulipaji wa tozo.

“Kumekuwa kweli kuna tozo mbalimbali zinatozwa na kumekuwa na kelele huko nyuma za wanaofanya biashara hii ya utalii wakilalamikia baadhi ya tozo, niipongeze sana serikali kwak uondoa baadhi ya tozo maana watoa huduma wameanza kufaidika na kazi nzuri ya serikali,

“Lakini bado tunaomba mkae na watoa huduma hawa ambao wanafanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha wanasimamia na kuwaleta watalii, lakini wanaomba kuwepo na dirisha moja la kuweza kulipa tozo,”amesisitiza.

Amesema kwa sasa mlolongo uliopo unawapotezea na hivyo kuomba wizara iangalie namna ya kupunguza mlolongo huo.

“Kumekuwa na mtawanyiko wa ofisi wa kulipia tozo hali inayowapotezea muda,mtu anaweza kuwa na tozo hata 50 na akatumia siku tatu hadi nne anashughulikia tu kulipa mgeni mmoja,hali hii inapoteza muda na inachelewesha sana kufikia lengo la kupata watalii wengi,”amesema.

Ushauri wa pili alioutoa ni kwenye suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

“Suala la VAT kweli hakuna anayekataa kulipa lakini kumekuwa na tatizo la kulipa VAT on deposit anapolipa mgeni nje analipa moja kwa moja kwa mtoa huduma ,mtoa huduma yule anakuwa anakatwa pale pale lakini ikitokea huyu mtalii ameahirisha safari ile VAT analipa huyu mwenzetu wa Tanzania maana yake anaingia hasara na anaitia hasara kampuni yake,

“Niombe fedha hizi zilipwe kwenye deposit lakini waje walipe kwenye maeneo ya tozo mbalimbali hiyo utakuwa umemtendea haki huyu mtoa huduma lakini pia itakuwa ni halisia,unaweza jikuta unalipia VAT mara mbili mara tatu kitu ambacho kinafanya destination ya Tanzania inakuwa ghali kuliko eneo lolote,hili nalo itakuwa ni kikwazo katika kupata watalii wa kutosha,”amebainisha.

Suala lingine ni kuhusu VISA kwa njia ya mtandao ambapo kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshaji.

“Malalamiko yamekuwepo kwamba mtu anapolipia Visa online kumekuwa na ucheleweshaji sana, ipo slow,na mtu yupo kule anataka kulipia ili apate ruhusa ya kukata tiketi lakini anashindwa matokeo yake anaamua kuahirisha safari au anaamua kutafuta eneo lingine,”ameongeza.

Mtaturu ametaja eneo lingine analoshauri ni uvamizi wa tembo katika maeneo ya watu na hivyo kuishauri wizara kupitia wataalam wake kutafuta mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

“Mimi naomba nitoe pole sana kwa wananchi wangu wa Ikungi singida Mashariki kwenye kijiji cha Ntewa pale Ntuntu, juzi alikanyagwa mtoto wa miaka miwili na nusu na tembo,eneo la Ikungi ni mbali sana na hifadhi lakini leo hii tunaongea habari ya Ikungi kuwa na uvamizi wa tembo na hapa mnatuambia tembo wapo karibia 60,000 na mnasema ni wachache ,je wakifika 100,000 au 200,000 itakuwaje nchi hii,?amehoji.

Amesema ni vyema wataalam wa wizara wakae watafute mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo.

“Wasijwe wakatuletea story iliyozoeleka mapito ya korido, mapito ya tembo ya miaka nenda rudi ,leo hii watu wengi wanaumia wanakufa, mali zao zinaharibiwa kwa sababu tu tembo anazunguka kila mahali ,inawezekana kuna mazao wanahitaji kula ,inawezekana maji hakuna maeneo ya hifadhi,basi wataalam wetu watumike kupanda hata miti ,wachimbe mabwa ya kutosha kwenye hifadhi ili tembo wasije kwa watu,

“Hii ndio maana ya kuwa na watu professional ,tuna wataalam wengi katika wizara hii, tunawaamini hebu nendeni mkakae mnapofanya utafiti fanyeni na eneo hili tusibaki kuleteana story kwamba ooh hii ni mapito ya tembo,tunajiuliza kule Ntuntu kule walikuwa wanaenda wapi,tembo wamekaa wiki nzima wiki mbili wanawafanya wananchi washindwe kufanya shughuli zao za kawaida,”amesema.

Amesema kila siku wanahamasisha wananchi wafanye kazi lakini kwa hali hiyo hawataweza kwa sababu ya uwepo wa tembo vamizi wanaozunguka ambao ni hatari kwa maisha yao.

“Niombe anapokuja waziri hapa atueleze mkakati ni upi wa kitaalam sio hoja hii ya kila siku imekuwa kama msamiati ambao haueleweki ,haya ni mapito sijui korido lugha nyingine zinawasumbua wananchi hawajui ,kwa hiyo niombe sana pamoja na kazi nzuri mnayofanya lakini eneo hili linatutia doa ,kama Taifa twendeni tukafanye kazi kwa pamoja,”ameomba.

About the author

mzalendoeditor