Featured Kitaifa

WAZIRI AWESO:’SERIKALI KUANDAA BEI ELEKEZI ZA MAJI ZITAKAZOTUMIKA MAENEO YA VIJIJINI’

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na kumpongeza Rais Samia kwa kuipatia wizara hiyo zaidi ya asilimia 95 ya fedha ilizoomba katika bajeti yake jijini Dodoma.

SEHEMU ya Watumishi wa Wizara ya Maji wakimsikiliza Waziri wa Maji Jumaa Aweso,(hayupo pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na kumpongeza Rais Samia kwa kuipatia wizara hiyo zaidi ya asilimia 95 ya fedha ilizoomba katika bajeti yake jijini Dodoma.

……………………………………………..

Na Bolgas Odilo, Dodoma

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,amesema kuwa Serikali inaandaa bei elekezi za maji zitakazotumika maeneo ya vijijini ili kuwezesha kila Mtanzania kupata huduma hiyo.

Waziri Aweso ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na kumpongeza Rais Samia kwa kuipatia wizara hiyo zaidi ya asilimia 95 ya fedha ilizoomba katika bajeti yake.

Aweso amesema kuwa erikali inapanga kuandaa bei elekezi za maji ambazo zitasaidia kuondoa kero ya gharama kubwa za maji katika maeneo ya vijijini.

“Ndoo ya maji maeneo ya vijijni ni Sh. 50 wakati mjini kama pale Dar es saalam mtu analipa unit moja ya maji kwa Sh.1500 lakini ukipiga kwa bei ya Sh. 50 ya mtu wa kijiji unapata Sh. 2500 kwa unit moja hivyo hii inamaanisha kuwa mtu wa mjini pale Dar analipa ndoo moja ya maji kwa Sh.30.

“Hivyo tunapanga kuleta bei elekezi hizi ambazo zitakwenda kuondoa kero hii na bei hizi zitaonyesha kuwa mtu ambaye anachota maji katika chanzo kinachoendeshwa kwa umeme ni bei gani,chanzo kinachotumia sola bei gani lakini pia kinachotumia mafuta bei gani ili kuondoa adha na kila mtu afurahie bei rahisi na nafuu za maji na kunufaika na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita”amesema Aweso

Hata hivyo Aweso amesema kuwa  wizara yake itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji safi na salama na yakutosheleza yanapatika katika maeneo yote ya mijini na vijijini.

“Tunakwenda kujenga miradi ya maji 175 mijini lakini pia tunakwenda kujenga miradi ya maji 1163 vijijini na hakuna sababu ya miradi ya maji kutumia muda mrefu kukamilika.

“Utekelezaji wa miradi ya maji usianze kusubiri subiri, michakato ambayo inahusiana na manunuzi juu ya utekelezaji wa miradi hii ya maji ianze sasa hivi ili tusicheleweshe huduma za upatikanaji wa maji kwa wananchi.

“Michakato yote ikamilike sasa ili tunavyoingia kwenye mwaka mpya wa bajeti tuanze utekelezaji wa miradi hiyo mara moja,” amesema Aweso.

Pia Aweso ameitaka mamlaka inayohusika na uunganishaji wa maji kwa wananchi kuzingatia mkataba uliowekwa baina ya mamlaka na mteja ili kutoa huduma kwa wakati.

“Mwananchi anatakiwa kuunganishiwa maji ndani ya siku saba kwahiyo mamlaka zetu za maji zihakikishe mwananchi anapoomba kuunganishiwa maji aunganishiwe kwa wakati kwa mudsa usiozidi siku saba.

“Tunawaomba viongozi mikoani na wilayani pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanaitunza miradi ya maji kwa kuwa inatumiwa na sisi ili tuendelee kupata maji safi salama na yakutosheleza.

“Na tutatoa bei elekezi kwa wananchi juu ya upatikanaji wa maji, kwa mfano anayetumia maji kwa kupitia nishati ya sola atakuwa na bei yake, atakayekuwa anatumia mafuta ya diesel bei yake na atakayekuwa anatumia nishati ya umeme atakuwa na bei yake,” alisema Aweso.

Aliongezea, “Hayo ni maelekezo ya Muheshimiwa Rais katika kuhakikisha anampunguzia mzigo mzito mwananchi wa kijijini ili aweze kupata huduma ya maji kwa gharama nafuu. 

Sanjali na hayo Aweso amesema kuwa kama viongozi wa Wizara wamejipanga kusimamia na kufuatilia miradi yote ya maji ili kuhakikisha watanzania wanapata maji yaliyo safi, salama na yakutosheleza.

About the author

mzalendoeditor