WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro akiongea na mawakili wa serikali zaidi ya 600 wakati akifunga mafunzo yao yaliyotolewa na ofisi ya wakili mkuu wa serikali.
Wakili mkuu wa serikali Gabriel Malata akiongea katika mafunzo ya mawakili wa serikali yaliyofungwa leo jijini Arusha.
kati ya mawakili 600 wa serikali kati wakifuatilia jambo katika mafunzo yao yaliyofungwa rasmi leo Mei 26 na waziri wa Katiba na sheria Dkt Damas Ndumbaro.
……………………………………….
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Waziri wa Katiba na sheria Dkt Damas Ndumbaro amewataka mawakili wa serikali kutobweteka kutokana utendaji mzuri ulioleta maafanikio makubwa tangu kuanzisha kwa ofisi ya wakili mkuu wa serikali bali iwe sifa na chachu ya kuwafanya waendelee kufanya vizuri zaidi.
Dkt Ndumbaro ametoa rai hiyo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya mawakili serikali zaidi ya 600 kutoka wizara na taasisi mbalimbali yaliyotolewa na ofisi ya wakili mkuu wa serilikali ambapo alisema kuwa wamefanya kazi kubwa sana ikiwemo kuokoa fedha zaidi ya Trilioni kumi na ili kuendelea kufanya vizuri zaidi wanatakiwa kuongeza bidii na kuzingatia miiko ya kazi zao kwani kazi ya uwakili ni kazi yenye heshima Duniani.
“Ofisi hii ni moja kati ya ofisi changa kabisa katika wizara ya Katiba na sheria lakini ni taasisi ambayo tangu kuanzisha kwake imeifanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, utendaji wa kazi wa ofisi hii unaonekana bayana umeoko fedha nyingi na mali za serikali kwahiyo ofisi hii ni muhimu sana katika wizara yetu na serikali yetu, mnafanya kazi kubwa sana,” Alisema Dkt Ndumbaro
Alieleza kuwa ni lazima wajipange kuhakikisha wanaendelea vizuri na endapo wameelewa mada walizofundishwa vizuri na kwenda kuzitekeleza na kuziishi, wanakwenda kumaliza kabisa matatizo mengi na migogoro ambayo serikali inaingia.
“Kama wizara ya Katiba na sheria tutaendelea kuwapa ushirikiano kila itakapohitajika lakini pia tunatarajia kwamba mafunzo haya yataenda kuwa chachu ya utatuzi wa migogoro mbalimbali ya kisheria ambayo inaikabili serikali na taasisi zake pamoja na kwenda kupunguza mashauri kwenye mahakama na maeneo mengine ambayo serikali inakabiliana nayo,” Alisema Dkt Ndumbaro.
Alifafanua kuwa wakifanikiwa kutekeleza ipasavyo na mashauri yakapungua itaokoa gharama ambayo serikali inatumia lakini muhimu zaidi wataenda kutekeleza kazi yao ya kuishauri serikali ili isiweze kupata mashauri mbalimbali.
Sambamba na hayo aliwataka kuwa wakwanza kuziheshimu sheria pamoja na kupambana na Rushwa kwani wako kwenye mfumo wa kutoa haki na Rushwa ni adui haki hivyo ni lazima waepuke jambo hilo pamoja na kwamba kesi wanazoziendesha ni kubwa na zina majaribu mengi.
“Maadili yetu yanatuambia tuepuke Rushwa kwani itakufikisha pabaya na haina siri, utapokea kwa siri lakini matendo yako yataanza kujionyesha hivyo endeleeni kufanya kazi kwa kuzingatia maadili,”Alisisitiza.
Kwa upande wake wakili mkuu wa serikali Gabriel Malata alisema kuwa majukumu ya ofisi ya wakili mkuu wa serikali ni kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yote yanayohusiana serikali na taasisi zake yanayofunguliwa ndani na nje ya nchi pamoja na kuingilia kati na kuendesha mashauri yanayohusu serikali na taasisi zake hasa katika mashirika na kampuni ambazo serikali inakuwa ni mwahisa muhimu.
“Ofisi ya wakili mkuu wa serikali ni kiungo kati ya wizara ya Katiba na sheria na miimili yote mitatu ambapo kupitia mawakili hawa tumeendelea kuhakikisha kwamba tunaendesha na tunapunguza mashauri yote yaliyopo mahakamani na ambayo hayajafunguliwa ili kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi ya migogoro na mashauri,” Alisema Malata.