Featured Kitaifa Magazeti

MBUNGE MTATURU ALIA NA MAFAO YA WASTAAFU

Written by mzalendoeditor

SERIKALI imesema imefanya jitihada mbalimbali za kulipa Deni la Mfuko wa PSSSF ikiwa ni pamoja na kutoa Hatifungani ya Shilingi. Trioni 2.17 ambazo zitaimarisha mtiririko wa mapato na kuwezesha kutoa mafao kwa wakati

Aidha,imesema wanufaika 42,427 wa Mfuko wa PSSSF wamelipwa jumla ya Sh. trilioni 1.99.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 24, na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu(CCM).

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya kuchelewesha mafao kwa wastaafu?.

Akijibu swali hilo Katambi amelihakikishia bunge kuwa serikali itaendelea kuwalipa wastaafu mafao yao.

“Kuanzia Julai 1, 2021 hadi Aprili 30, 2022, wastaafu na wanufaika 24,757 wa Mfuko wa NSSF wamelipwa jumla ya Sh. bilioni 78,”.amesema.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo amesema pamoja na majibu ya serikali kuhusiana na wastaafu kulipwa mafao kwa wakati kumekuwa na malalamiko ya kuchelewa kulipwa mafao yao mapema na malalamiko makubwa ni baadhi ya wastaafu kukatwa makato ambayo hayapelekwi kwenye mifuko hiyo.

Kutokana na changamoto hiyo, amehoji, Nini kauli ya serikali kwenye eneo hili kwa sababu imekuwa na usumbufu mkubwa usio na lazima kwa kuwa wamekuwa na mtumishi katika miaka yote.

Aidha, amesema wastaafu wamekuwa wakiombwa taarifa zao upya baada ya kuwa wameshastaafu serikali inakuwa ina taarifa zao zaidi ya miaka 30 na kuhoji kama haioni kwamba ni usumbufu wa kuwaomba wastaafu ambao wamekuwa nao miaka yote ya umri wao,”amehoji.

Akijibu swali hilo, Katambi amefafanua kuwa tayari wameshafanyia kazi suala hilo na maelezo yalishatolewa ndani ya bunge na aliyekuwa waziri mwenye dhamana wakati huo Jenista Mhagama na wa sasa Profesa Joyce Ndalichako.

“Tayari tathimini na mapitio yameanza kufanyika upya ili kuhakikisha kwamba wanalipwa kwa wakati na tayari kuna mifumo mbalimbali ya kitehama ambayo imeanzishwa hii yote ni kwa ajili ya kutengeneza ile membership administration service system.

Mbali na hayo amesema hivi karibuni wataanza ziara ya mkoa kwa mkoa kuanza kusikiliza changamoto za wastaafu ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa mbalimbali ili kuhakikisha wanalipwa kwa wakati.

“Utakumbuka kwenye bunge lako hili tulitoa taarifa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kwamba ili suala la uombaji wa barua za wastaafu limefikia mwisho kwa sababu taarifa hizi ni wajibu sasa wa mifumo yenyewe kuweza kuhakikisha zinatunza kumbukumbu sahihi za wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuanzisha ndani ya huo mfumo wa membership pamoja na mfumo wa NSSF wenyewe, yote hii taarifa zitakuwa mle,”.

Ametumia nafasi hiyo kuwasihi waajiri kote nchini kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati ili wasihangaike,pia kuhakikisha mfuko wenyewe unahakiki taarifa za wale wastaafu hata mwaka mmoja kabla ya kustaafu ili kupunguza usumbufu kwa watumishi hao ambao wametumikia Taifa.

About the author

mzalendoeditor