Featured Kitaifa

SERIKALI YAIBAINISHI KUIVA KWA MKAKATI WA TAIFA KUJENGA UCHUMI WA KIDIGITALI

Written by mzalendoeditor
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeweka bayana kuwa imekamilisha uandaaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali utakaochochea matumizi ya TEHAMA katika sekta zote za uchumi Tanzania.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari bungeni Dodoma, Waziri Nape Moses Nnauye amebainisha kuwa katika kufikia azma hiyo serikali kupitia wizara hiyo tayari imekamilisha uandaaji wa Mwongozo wa Mageuzi ya Kidijitali (Digital Transformation Guideline) utakaoongoza taasisi zote nchini katika kujenga uchumi wa kidijitali;
“Eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mheshimiwa Mwenyekiti katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekamilisha uandaaji wa rasimu ya Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy Strategic Framework) kwa ajili ya kuchochea matumizi ya TEHAMA kwenye sekta zote za uchumi.”
Aidha, kwa kuzingatia kwamba uchumi wa Kidijitali unaenda sambamba na upatikanaji wa huduma za mtandao Zenye uhakika na ubora Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa intaneti yenye kasi (National broadband Strategy) sambamba na kuingia makubaliano na Shirika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya kufanya kazi pamoja ya kupitisha miundombinu ya mawasiliano kwenye nguzo za umeme kwa lengo la kuongeza mtandao wa mawasiliano na wa umeme.
Nape amefafanua kuwa, hatua ya kushirikiana na TANESCO kusambaza Miundombinu ya mawasiliano imepunguza gharama za ujenzi wa Mkongo na kuharakisha mradi huo ambapo mipango ya awali zilikuwa zijengwe kilomita 1,880 lakini kutokana na Mkataba wa mashirikiano na Shirika hilo sasa zitajengwa Kilomita 4,442 na kufikisha jumla ya Kilomita 12,761 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ujenzi utakapokamilika Mwezi Disemba, 2022;
Alisisitiza kuwa, ili kujenga uchumi thabiti wa kidijitali unaoendana na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th Industrial Revolution). “Serikali itahakikisha uandaaji wa Programu ya Mafunzo ya TEHAMA yatakayowezesha kuongeza ujuzi na ubobezi wa wataalamu wa ndani ili kuendana na mahitaji ya sasa ya Uchumi wa Kidijitali kufikia unatekelezwa kwa kadri ilivyopangwa” alisisitiza Nape.
Katika kufikia azma ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaolenga kuleta mabadiliko ya Kidijitali kwa kuwezesha maunganisho ya Kidijitali ya Kikanda na Kimataifa na hatimaye kukuza Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy) Serikali imebainisha kuwa itaendelea kutekeleza mradi huu ili kuongeza na kubuni ajira zitakazotokana na ubunifu wa TEHAMA, ukuzaji wa viwanda vidogo vidogo (SMEs na SMMEs); kukuza ustadi wa wataalamu wa ndani ya Serikali na waliopo nje ya Serikali; na kuongeza uwezo wa utoaji wa Huduma za Serikali kwa kuwezesha uwepo wa intaneti bora ya bei nafuu na ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya Serikali ili kumnufaisha mwananchi.

About the author

mzalendoeditor