Featured Kitaifa

TAASISI YA WANAWAKE 100 ,000 YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UJASIRI WA KIPEKEE KUONGEZA MISHAHARA, KUDHIBITI BEI YA MAFUTA NA THE ROYAL TOUR

Written by mzalendoeditor

 

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake 100,000 (kulia), Vicky Kamata akiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyatt jujini Dar es Salaam leo akipongeza ujasiri wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kuleta ahueni kwa Watanzania kufuatia ongezeko la bei za mafuta duniani. Kushoto ni Josephine Matiro, Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000.
Balozi wa Utalii Tanzania na Mkurugenzi wa Miradi, Taasisi ya Wanawake 100,000 (katikati), Nangasu Warema akiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mwenyekiti wa Wanawake 100,000 Vicky Kamata na kushoto ni Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000, Josephine Matiro. Viongozi hao wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushujaa wa kipekee katika kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa 23.3%, kuchukua hatua za dharura dhidi ya bei ya mafuta duniani na kutangaza utalii na uwekezaji Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour.
Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000 (katikati) Josephine Matiro akiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Balozi wa Utalii Tanzania na Mkurugenzi wa Miradi, Taasisi ya Wanawake 100,000 Nangasu Warema, kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake 100,000 (kulia), Vicky Kamata.
 
  **
 
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanawake Laki Moja ‘Wanawake 100, 000’ imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri wa kipekee, ubunifu na uthubutu wake katika kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa 23.3% kwa watumishi wa umma, kuchukua hatua za dharura kudhibiti bei ya mafuta duniani na kutangaza utalii na uwekezaji Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour.
 
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 20,2022 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Laki Moja, Vicky Kamata amesema Taasisi yao inampongeza Rais Samia kwa uongozi wake wa kishujaa, kumtia moyo aendelee na jitihada zake na kumhakikishia kuwa Watanzania wapo pamoja naye bega kwa bega kukabiliana na changamoto za maendeleo nchini.
???
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WANAWAKE TANZANIA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UJASIRI
WA KIPEKEE 
 
Dar es Salaam, Mei 20, 2022
 Ifuatayo ni taarifa kwa vyombo vya habari nchini Tanzania kutoka kwa taasisi isiyo ya
kiserikali ya Wanawake 100,000.
 
 Taasisi yetu inawakilisha wanawake zaidi ya 100,000
kutoka kila kona ya nchi yetu na pia tunasimama hapa kwa niaba ya Watanzania wote
nchini wanaopenda maendeleo ya taifa letu. 
 
Ndugu wanahabari, leo tumewaita hapa kuzungumzia masuala matatu makuu ambayo
kwa sasa yameibua mijadala mbalimbali kwenye jamii, hususan nyongeza ya kima
cha chini cha mshahara cha asilimia 23.3% iliyotangazwa na serikali hivi karibuni,
jitihada za serikali kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta duniani na uzinduzi wa
makala maalumu ya The Royal Tour uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi
karibuni Marekani na nchini Tanzania. 
 
Tungependa kuchukua fursa hii kutoa pongezi za dhati kwa Rais Samia
kuonesha ujasiri wa kipekee, ubunifu na uthubutu katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali zilizotokea nchini na duniani kwa ujumla tangu achukue uongozi wa nchi
mwezi Machi mwaka jana (2021).
 
 NYONGEZA YA MSHAHARA
 
 Mnamo tarehe 14 Mei 2022, taarifa iliyotolewa na Ikulu ilitangaza kuwa Rais Samoa
ameridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara, ikiwemo kima cha chini kwa
watumishi wa umma kwa asilimia 23.3 na hivyo kuibua shangwe kubwa nchini.
 
 Ongezeko hili la mshahara ni kubwa kuwahi kutokea nchini kwa kipindi kirefu sana. Kwa miaka mingi sasa, wafanyakazi nchini wamekuwa na kilio cha kutoongezwa
mshahara na kutopandishwa vyeo kwa watumishi wa umma. 
 
Vile vile, mifuko ya pensheni nchini ilikumbwa na uhaba mkubwa wa fedha na hata
kushindwa kulipa mafao kwa wakati kutokana na serikali kuwa na malimbikizo
makubwa ya michango ya penchent ya watumishi wa umma. 
 
Ndani ya mwaka mmoja tu, Rais Samia ameweza kuongeza mshahara kwa 23.3%,
amepandisha watumishi wa umma madaraja na kulipa malimbikizo ya mchango wa
pensheni za watumishi wa umma.
 
 Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi trilioni 9.7 katika mwaka wa fedha ujao
wa 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishara ya watumishi wa umma.
 
 Hili ni
ongezeko la Shilingi trilioni 1.59 ukilinganisha na bajeti ya 2021/22.
 
 Ongezeko la kima cha chini cha mishahara pamoja na kupandishwa kwa madaraja kwa
watumishi wa umma, siyo jambo jema kwa watumishi wa umma pekee, bali taifa zima.
 
 Maelfu ya walimu, manesi, askari na watumishi wa kada nyingine wataongeza kipato
chao na mafao yao kutokana na ongezeko hili.
 
 Utafiti wa wachumi huonesha pia kuwa ongezeko la mshahara huleta chachu kwenye
jamii yote, huongeza pato la taifa la hukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
 
 
 UDHIBITI WA BEI YA MAFUTA NCHINI 
 
Kama mnavyofahamu, hivi karibuni nchi mbalimbali duniani zimekumbwa na
msukosuko wa kupanda kwa bei za mafuta kutokana na vita inayoendelea sasa hivi
nchini Ukraine. 
 
 
Tanzania siyo Kisiwa na yenyewe pia inakabiliana na changamoto zitokanazo na bei ya
mafuta kupanda ghafla kwenye soko la dunia na hivyo kuleta athari katika mfumuko wa
bei, gharama za uzalishaji kwenye uchumi na kuongeza ugumu wa maisha kwa
wananchi mijini na vijijini.
 
 Kwa ujasiri wa kipekee, Rais Samia ametoa maelekezo kwa serikali yake
kuchukua hatua za dharura kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta duniani
kabla ya mwaka ujao wa fedha wa 2022/23.
 
 Badala ya kusubiri hatua za kikodi kwenye bajeti ijayo ya serikali ambayo utekelezaji
wake utaanza Julai 1, 2022, Rais Samia ameagiza kuwa ahueni itafutwe mapema zaidi
kwa kutoa maelekezo kwamba katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa
fedha, Serikali ijibane na ijinyime na itolewe ruzuku ya shilingi bilioni mia
moja (Shilingi 100,000,000,000) kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini. 
 
 Kiasi hiki cha ruzuku kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta duniani hakijawahi
kutolewa na serikali ya Tanzania tangu tupate uhuru, lakini kwa ujasiri wa kipekee, Rais
Samia ameiagiza serikali yake kufanya maamuzi hayo magumu ya dharura.
 
 
 Ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya serikali (yaani recurrent expenditure)
katika kipindi kilichobaki cha mwaka wa feda wa 2021/22.
 
 
 Fedha za miradi ya
maendeleo hazitaguswa na zitaendelea kutolewa kama ilivyopangwa. Ruzuku hii ya
shilingi bilioni 100 itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei kuanzia tarehe 1 Juni 2022.
 
 Pamoja na ruzuku, Rais Samia ameiagiza serikali yake kuchukua hatua nyingine zisizo
za kifedha kuleta ahueni kwa wananchi dhidi ya ongezeko la bei ya mafuta duniani.
 
 Hatua hizo ni pamoja na kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu
kufanya hivyo, kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za mafuta, Kuanzisha Hifadhi
ya Mafuta ya Kimkakati na Serikali kukamilisha makubaliano ya kujenga maghala
makubwa ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya kuuzwa ndani na nje ya nchi kulingana na
uhitaji.
 
 Hatua nyingine zinazochukuliwa na serikali ni pamoja na kuanzisha upokeaji wa
mafuta katika ghala moja kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama
za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala
mengi, Kuiongezea uwezo TPDC kuagiza mafuta nje ya nchi na kuimarisha utendaji na
weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo
EWURA na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja. 
 
Wakati mataifa mbalimbali duniani yamekumbwa na tafrani kutokana na sakata la bei la
mafuta, ikiwemo changamoto za foleni na vurugu katika vituo vya mafuta kutokana na
uhaba wa mafuta, kumekua na utulivu mkubwa nchini Tanzania, bila uhaba wa mafuta
nchini kutokana na hatua za dharura za kijasiri za serikali chini ya uongozi wa kijasiri wa
Rais Samia. 
 
Leo hii, mamilioni ya Watanzania wanapata ahueni na wataendelea kupata ahueni zaidi
kuanzia Juni 1 na July 1 wakati hatua zisizo za kibajeti na za kibajeti zitakapoanza
kuleta matunda.
 
 Sisi Wanawake 100,000 tumezungumza na wafanyakazi, wakulima, wavuvi,
wafanyabiashara, madereva wa bodaboda, Bajaji na daladala, mama ntilie na wananchi
wote nchini na wote wanaungana kumpongeza Rais Samia kwa ujasiri wa kipekee
alionesha katika kukabiliana na tatizo la ongezeko la bei ya mafuta duniani.
 
 
 KAMPENI YA THE ROYAL TOUR
 
 Bila kumumung’unya maneno, The Royal Tour ni ubunifu na jitihada kubwa za kutangaza
fursa za Utalii na uwekezaji nchini ambazo hazijawahi kutokea tangu tupate uhuru
takribani miaka 60 iliyopita. 
 
Sote tunafahamu namna ambavyo nchi jirani zimekuwa zikitumia mabilioni ya pesa
kutangaza utalii wao duniani huku Tanzania ikiachwa nyuma hadi kupelekea baadhi ya
watu huko nje kulaghaiwa kuwa Mlima Kilimanjaro na hata Serengeti ziko nchi jirani na
siyo Tanzania.
 
Lakini kwa kupitia ushiriki wake kwenye Filamu ya The Royal Tour, Rais Samia amewezesha
kuitangaza Tanzania kimataifa na kupeperusha bendera ya nchi. 
 
Ni vyema kusisitiza kuwa The Royal Tour siyo movie kama zile zinazotengenezwa
Hollywood au Bollywood au Nollywood au Bongo movie. 
 
The Royal Tour ni makala malumu
inayotoa fursa ya kipekee na mahsusi ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni kama
kitovu cha utalii na uwekezaji duniani. 
 
Wakati watu wengine wanakaa ofisini kwenye viyoyozi, Rais Samia alifanya kazi
ngumu kuongoza kurekodiwa kwa documentary hii porini na hata kushinda bila kula
wakati mwingine kuhakikisha kuwa nchi yake aipendayo sana ya Tanzania inatangazwa
ulimwenguni. 
 
Kama alivyosema Rais Samia mwenyewe, gharama ya kurekodi filamu ya The Royal Tour
na kuitangaza duniani zimelipiwa na michango kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali
nje na ndani ya sekta ya utalii nchini. 
 
Tukiwa kama wadau wa utalii, tunatoa pongezi za dhati kwa jitihada binafsi za Rais Samia
na mchango mkubwa wa wafanyabiashara na taasisi mbalimbali nchini zilizofanikisha The Royal Tour na kuipaisha Tanzania kimataifa duniani. 
 
Ni makala maalum inayohusisha Wakuu wa Nchi waliopo madarakani ili kuzieleza nchi
zao na kuzitangaza kimataifa katika sekta mbalimbali. 
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hive karibuni na Bi. Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Tanzania ni miongoni mwa nchi ya 9 kushiriki programu hii
ya The Royal Tour ambayo pia humpa nafasi kiongozi husika kuzindua makala hayo nchini
Marekani, kupata nafasi ya mahojiano na vyombo vikubwa vya habari na kukutana na
wadau mbalimbali wa biashara, utalii na uwekezaji ana kwa ana ili kuwavutia kuja nchini
kuwekeza.
 
 Nchi nyingine zilizoshiriki kampeni ya The Royal Tour ni Jordan, New Zealand, Poland,
Mexico, Ecuador, Peru, Israel, Rwanda na sasa Tanzania.
Sababu nyingine ya kutumia Marais walio madarakani kwenye programu hiyo ni
kujenga imani kwa watazamaji, yaani watalii na wawekezaji.
 
Tayari filamu hii imefanikiwa kuitangaza Tanzania kimataifa na itaendelea kufanya hivyo
kwa miaka mingi ijayo kwani imewekwa pia inapatikana katika mitandao mikubwa
duniani kama Amazon na Apple TV na itaoneshwa katika chaneli 350 nchini Marekani
5
zinazowafikia Wamarekani zaidi ya milioni 200.
 
 Katika siku zijazo, Tanzania linatarajia kupokea wawekezaji na watalii wengi kutokana
na jina la nchi yetu sasa kuwa gumzo duniani kupitia ushiriki wa Rais Samia kenye
makala maalumu ya The Royal Tour. 
 
Kama tulivyosema awali, lengo la taarifa yetu hii ni kumpongeza Rais Samia kwa
uongozi wake wa kishujaa, kumtia moyo aendelee na jitihada zake na kumhakikishia
kuwa sisi Watanzania tuko pamoja naye bega kwa bega kukabiliana na changamoto za
maendeleo chini. 
 
Ahsanteni kwa kutusikiliza.
 
 Imetolewa na:
 Vicky Kamata, Mwenyekiti wa Wanawake 100,000
 
 Nangasu Warema, Balozi wa Utalii Tanzania na Mkurugenzi wa
Miradi, Wanawake 100,000
 
 Josephine Matiro, Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000
 

About the author

mzalendoeditor