NAIBU Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa,akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo kilichopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Kiruswa akiwa na wachimbaji wadogo wa madini Mkoani Singida
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo kilichopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Chone Malembo akizungumza wakati wa ziara ya Dkt. Kiruswa Mkoani Singida
Wachimbaji wadogo wa madini katika Kijiji cha Matongo wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini
***************************
NAIBU Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemwagiza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini kwa wachimbaji wadogo wa madini ili waendeshe shughuli zao kwa kufuata Taratibu, Sheria na Kanuni za Madini.
Dkt. Kiruswa ametoa maagizo hayo Mei 14, 2022 alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo kilichopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.
Amepokea malalamiko kutoka kwa wachimbaji wa Kijiji cha Matongo ambapo wamemweleza kuwa hawaelewi Sheria za Madini zilizopo jambo linalowapa changamoto katika utekelezaji wa shughuli za uchimbaji katika maeneo yao.
Aidha, ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuhakikisha wanafanya utafiti katika kijiji hicho ili wachimbaji wachimbe kwa tija.
Wakati huo huo, Dkt.Kiruswa ametoa wito kwa taasisi za kifedha zikiwemo benki watembelee eneo hilo na maeneo mengine ili waweze kutoa elimu ya kutosha kwa wachimbaji wa madini kuhusu namna ya kupata mikopo na utunzaji wa fedha.
Akizungumzia migogoro ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo, Dkt. Kiruswa ametoa muda wa wiki mbili kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Madini ya Mkoa kuhakikisha wanamaliza migogogro yote ikiyowasilishwa na wananchi wakati wa ziara hiyo.
Akizungumzia ukosefu wa umeme na maji katika migodi hiyo na ubovu wa barabara inayoelekea mgodini hapo, Dkt.Kiruswa amesema, Serikali itaboresha mazingira hayo ili wachimbaji hao waweze kuchimba na kupata manufaaa.
Amesema, Serikali ni sikivu na itahakikisha inatatua changamoto hizo kwa wakati ili waendelee na uchimbaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameomba ofisi na GST wasogeze huduma za kitafiti katika maeneo hayo ya wachimbaji ili waweze kuchimba kwa tija.
Amesema, wachimbaji hao kwa sasa wanachimba kwa kubahatisha jambo linalofanya wapoteze fedha nyingi.
Vilevile, Mtaturu ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini iweze kuwasaidia wachimbaji hao kupata mitaji ili iwasaidie kuweza kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa vya uchimbaji kuendana na teknolojia.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Chone Malembo ametumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji kushirikiana na Ofisi ya Madini Singida ili waweze kutatua migogoro yote inayowasumbua wachimbaji.
Aidha, ameeleza kuwa wamepokea maelekezo ya Naibu Waziri na wamejipanga kuyatekeleza kwa kutoa elimu kuhusu Sheria na Kanuni za Madini pamoja na uchimbaji wenye tija ili wachimbaji waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi.
Aidha, amewataka kuzingatia sheria na kanuni zote za uchimbaji ili kuepusha migogogro inayojitokeza mara kwa mara na kusababisha wachimbaji hao kutumia muda mwingi katika kuitatua badala ya kutumia muda huo katika shughuli za uchimbaji.
Naibu Waziri wa Madini amefanya ziara ya siku mbili mkoani Singida ili kuzungumza na kusikiliza kero mbalimbali zinazowasumbua wachimbaji wadogo.