Featured Kitaifa

MBUNGE PINDA AWEZESHA WANANCHI WAKE KUPATA PAWATILA 53

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Anthony Mavunde amekabidhi jumla ya matrekta ya mkono maarufu kama pawatila 53 zilizotolewa kwa kwa mkopo kwa Vyama vya Msingi vya wakulima (amcos) katika Jimbo la Kavuu lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Matrekta hayo yaliyotolewa kwa mkopo nafuu baada ya juhudi za Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Mhe Geophrey Pinda kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo zitasaidia kukuza na kuendeleza kilimo katika eneo hilo linalolima mazao mbalimbali kama mpunga, mahindi, alizeti na mazao mengine.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Anthony Mavunde ameziagiza taasisi za fedha lnchini kuhakikisha zinakuwa na masharti rahisi na rafiki kwa wakulima pindi wanapotaka kukopa ili kuendeleza sekta ya kilimo.

Mhe Naibu Waziri Mavunde alisema kuwa masharti hayo yatakapopungua wakulima wengi wataweza kukopa na kufanya kilimo cha kisasa zaidi na kufanikisha kukuza pato la mkulima nan chi kwa ujumla.

“Tuzipongeza benki kwa kupunguza riba kwa wakulima kutoka asilimia 22 mpaka chini ya asilimia 10 kwa baadhi ya mabenki lakini pamoja na kupunguza riba pia muangalie eneo lingine la masharti. Lazima muweke masharti mepesi ya kufanya mkulima akopesheke.

Hivi sasa tumetoa maelekezo na kuzishauri benki ziingie katika mfumo wa mikataba ya utatu. Mkataba wa mkulima na mnunuzi utumike kama dhamana badala ya mkulima kutakiwa kuweka dhamana ya nyumba,” alisema Mhe Mavunde.

Mhe Mavunde alisema kuwa mfumo huo umefanyiwa majaribio katika baadhi ya maeneo na umeonyesha matokeo mazuri na benki zimekuwa na uhakika wa fedha zao kurudi.

Awali akimkaribisha Mhe Naibu Waziri Mavunde, Mbunge wa Kavuu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Geophrey Pinda amesema kuwa mkopo huo utawasaidia wakulima kuweza kulima kisasa na kuondokana na kilimo cha jembe la mkono.

About the author

mzalendoeditor