Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO AONGOZA MATEMBEZI MAADHIMISHO YA RED CROSS

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiongoza matembezi ya ya hisani kuanzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma hadi Ukumbi wa Vijana Wajenzi katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Red Cross l

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya ukumbi wa Vijana Wajenzi jijini Dodoma mara baada ya matembezi ya hisani yaliyoanzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Red Cross leo Mei 8, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipanda mti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Red Cross leo Mei 8, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na washiriki wa Maadhimisho ya miaka 60 ya Red Cross wakati wa zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa

……………………………………………………..

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameongoza zoezi la upandaji miti na matembezi ya hisani katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Red Cross leo Mei 8, 2022 jijini Dodoma.

Zoezi la upandaji miti limefanyika katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo matembezi hayo yameanzia katika eneo hilo hadi ukumbi wa Vijana uliopo eneo la Wajenzi.

Akizungumza na washiriki wa maadhimisho hayo na wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi la upandaji miti sambamba na matembezi hayo, Dkt. Jafo alisisitiza kuwa ili tuwe na utalii endelevu hatuna budi kuhifadhi mazingira.

Aliipongeza Red Cross kwa maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na zoezi la upandaji miti jambo ambalo linaonesha dhamira ya kutekeleza maelekezo ya Serikali katika ajenda ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Nimefarijika kuona mna mipango ya kuhakikisha mnakwenda sambamba na maelekezo ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akielekeza suala zima la utunzaji mazingira na mnafahamu leo kuna uzinduzi wa filamu ya Royal Tour ambayo itatusaidia katika uwekezaji wa utalii na nyie mnachokifanya mnaongeza thamani ya kile Mama anachokifanya,” alisema.

Pia Waziri Jafo aliwataka kuadhimisha maadhimisho hayo wakitambua kuwa wana kila sababu ya kujenga uchumi na amani ya nchi na kusema hayo yote yatafanikiwa kama mazingira yakilindwa.

“Ndugu zangu tunaadhimisha miaka 60 ya Red Cross huku tukiuonesha ulimwengu kuwa tunajali mazingira wakati tunapopanda miti kama tunavyofanya hapa kwenye Hospitali ya Mkoa.

Kwa upande wake Rais wa Red Cross Tanzania Mhe. David Kihenzile alisema wanatambua mikakati ya Serikali katika suala la utunzaji wa mazingira hasa katika kampeni ya kupanda miti kwa kila halmashauri.

Kihenzile ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira alisema kuwa pamoja Red Cross imejipanga kupanda miti milioni 10 kwa kila mkoa ili kuiunga mkono Serikali katika utunzaji mazingira.

Aidha, alisema kwa mujibu wa Sheria namba 71 ya mwaka 1972 kazi ya Red Cross ni kutoa huduma kwa wananchi hususan wakati wa changamoto za kimazingira zikiwemo mafuriko na ukame.

About the author

mzalendoeditor