Featured Kitaifa

MBUNGE KUNAMBI ARIDHISHWA NA UJENZI WA BARABARA YA  MITA 750 KIWANGO CHA LAMI,AMSHUKURU RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi amekagua ujenzi wa Barabara ya Lami katika Tarafa ya Mlimba yenye urefu wa Mita 750 ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha kiasi cha Sh Milioni 409 kwa ajili ya ujenzi huo.

Akizungumza na wananchi wa Tarafa hiyo baada ya kukagua ujenzi huo, Kunambi amesema tayari pia Serikali imeshamuahidi kumpatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara nyingine ya lami ya Mita 450 ambayo pia itakua na taa za barabarani.

” Tumekagua wote ujenzi wa Barabara hii na tumeridhishwa na kiwango cha lami, kukamilika kwa Barabara hii ni muendelezo wa kuzidi kuboresha Tarafa yetu ya Mlimba ili izidi kukua kwani malengo yetu hapo baadae ni kuishawishi Serikali iweze kuitangaza Mlimba kama Mji Mdogo.

Hakika Rais Samia tangu aingie madarakani Jimbo letu la Mlimba analitazama kwa upekee wa hali ya juu, ametupatia Sh Milioni 409 ambazo zimetengeneza lami hii ya mita 750, kuweka kalvati na kuboresha mitaro ya barabara.

Kama hiyo haitoshi tayari Serikali umekubali kutupatia fedha ambazo zitajenga Barabara nyingine hapa ya mita 450 ambayo pia tunapambana kuhakikisha inapata na taa kabisa ili kuumulika mji wetu wa Mlimba watu wafanye biashara hadi usiku hapa,” Amesema Kunambi.

Kunambi amewataka wananchi wa Tarafa ya Mlimba na Jimbo hilo kwa ujumla kuendelea kuiunga mkono Serikali huku pia akiwasisitiza kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti mwaka huu.

About the author

mzalendoeditor