WAZIRI wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji,akizungumza leo Mei 6,2022 jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023.
……………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bidhaa muhimu hususa vifaa vya ujenzi,sukari,mafuta ya kula mbolea na bidhaa za chakula.
Imesema kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutumia mbinu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa hizo ili kukidhi mahitaji.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Mei 6, 2022 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo,Dkt.Ashatu Kijaji wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023.
Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu hususan zile zilizoonekana kuathiriwa na UVIKO-19 sambamba na vita kati ya Ukraine na Urusi.
Hivyo, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutumia mbinu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa hizo ili kukidhi mahitaji.
“Serikali imeendelea kuwaagiza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa bei ya soko,”amesema.
Pia amesema Serikali inawaelekeza wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji.
“Serikali inawaelekeza wazalishaji wa bidhaa muhimu kuzalisha na kusambaza bidhaa husika kulingana na uwezo wa viwanda uliosimikwa ili kukidhi mahitaji ya soko.
“Serikali inawaelekeza wauzaji na wasambazaji wa mbolea zenye bei elekezi wahakikishe wanazingatia bei zilizopangwa na Serikali na wale wote watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni za biashara; na
Waziri Kijaji ameilekeza Tume ya Ushindani (FCC) ifuatilie kwa karibu mwenendo wa biashara wa bidhaa muhimu ambazo katika tathmini iliyofanyika zimeonesha kuathirika zaidi na upandaji wa bei na kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kukiuka Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2003.
Amesema Serikali imeendelea kushawishi na kuvutia Wawekezaji wa ndani na nje kwenye uzalishaji wa mazao ambayo tumekuwa tegemezi kwa kiwango kikubwa kutoka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na mafuta ya kula, sukari na ngano.
Amesema lengo likiwa ni kupata uzalishaji unaotosheleza mahitaji ya soko letu la ndani na hatimaye kuuza nje kwa sababu hiyo tunayo kama Taifa.
VIWANDA VYASAMBAA NCHI NZIMA
Waziri Kijaji amesema uwekezaji katika Sekta ya Viwanda umeendelea kukua na kumilikiwa kwa sehemu kubwa na Sekta Binafsi.
Amesema uwekezaji huo wa viwanda uko katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZ na SEZ) na maeneo binafsi.
Amesema Viwanda vimesambaa nchi nzima na sehemu kubwa ya viwanda hivyo ni vidogo sana ambavyo ni 62,400 sawa na asilimia 77.07, wakati vidogo ni 17,267
sawa na asilimia 21.33, vya kati ni 684 sawa na asilimia 0.84 na vikubwa ni 618 sawa na asilimia 0.76.
“Kati ya Viwanda Vikubwa 618 (Vinavyoajiri kuanzia watu 100), Viwanda 41 pekee vinaajiri zaidi ya watu 500.Viwanda vingi vinajishughulisha na uongezaji thamani ya mazao
ya kilimo na vinajielekeza katika kutumia malighafi za ndani kuzalisha bidhaa hizo,”amesema.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 imefufua majadiliano ya mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Bagamoyo (BSEZ) uliosimama tangu mwaka 2018.
Amesema Wizara yake inaratibu uendelezaji wa BSEZ unaolenga kuendana na ushindani wa biashara za usafiri wa majini, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo viwanda na utalii.
Pia katika mwaka 2021/2022, wizara imefufua majadiliano na wawekezaji wa Kampuni ya China, Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Oman Investment Authority (OIA) ambayo awali ilikuwa inaitwa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (SGRF).
Amesema majadiliano hayo yanahusu eneo dogo la Mradi wa BSEZ kwa kuendeleza eneo la hekta 3,087 kati ya hekta 9,887 ambapo unahusisha ujenzi wa Bandari (Sea 38 Port).
Pia inahusisha ujenzi wa Kituo cha Usafirishaji kwenye eneo la hekta 887 na uendelezaji wa Eneo Maalum la Viwanda kwenye eneo la hekta 2,200.
“Msingi wa marejeo ya majadiliano hayo ambayo yalisimama mwaka 2018 ni kuhakikisha Serikali inatekeleza maeneo ambayo ni wajibu wake kama vile ujenzi wa miundombinu wezeshi (barabara, reli, umeme, maji, gesi na mifumo ya mawasiliano) na lango la kuingilia bandarini kwa maslahi mapana ya Taifa,”amesema.
Amesema uwekezaji katika maeneo ya Mradi yatafanywa kwa kuvutia wabia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) au kufanywa na mwekezaji binafsi.
Aidha, Dk Kijaji amesema wizara kupitia Shirika la Viwango Nchini (TBS) imezuia bidhaa zisizokidhi viwango kutoka nje ya nchi kuingia sokoni shehena 1,517 na limeteketeza bidhaa zisizo kidhi ubora zenye thamani ya Sh6.73 bilioni.
“Sehemu kubwa ya bidhaa zilizozuiwa na zilizoondolewa kutoka sokoni zilikuwa ni bidhaa za chakula na vipodozi. Hatua stahiki zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ikiwemo kuelimisha umma na bidhaa husika kuharibiwa,”amesema.
SHERIA
Waziri Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa amesema Wizara inafanya
marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuweka mazingira rafiki katika uwekezaji, viwanda na biashara.
“”Kwa sasa, Wizara inaendelea kufanya Marekebisho ya Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2003; Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997; Sheria ya Viwango ya Mwaka 2009; Sheria ya Leseni za Biashara Sura 208; na Sheria ya Vipimo Sura na 340 na mapitio yake ya mwaka 2002.
Sambamba na hilo, Wizara inaendelea na maandalizi ya Kutunga Sheria ya Ahueni ya Athari za Biashara ya Mwaka 2022 (Trade Remedies Act, 2022).
YAOMBA BILIONI 99
Katika Mwaka 2022/2023, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaomba kutengewa jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 99.
Amesema kati ya fedha hizo, Wizara inaomba kutengewa zaidi ya Shilingi bilioni 68 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 30,796,819,000 za Matumizi ya Maendeleo.
“Fedha za Matumizi ya Kawaida zinajumuisha Shilingi 8,728,788,000 za
Matumizi Mengineyo (OC) na Shilingi 59,579,899,000 za Mishahara,”amesema.
Aidha, Fedha za Matumizi ya Maendeleo zinajumuisha Shilingi 30,346,819,000 fedha za ndani na Shilingi 450,000,000 fedha za nje.