Featured Kitaifa

MAJALIWA AZINDUA MRADI WA USAID AFYA YANGU JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma kuzindua Mradi wa USAID AFYA YANGU  Mei 6, 2022. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright  na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,akizungumza wakati akizindua Mradi wa USAID AFYA YANGU kupitia ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) uliofanyika  leo Mei 6,2022 jijini Dodoma.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa USAID AFYA YANGU kupitia ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) uliofanyika  leo Mei 6,2022 jijini Dodoma.

Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya USAID AFYA YANGU kupitia ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) uliofanyika  leo Mei 6,2022 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa Bi.V.Kate Somvongsiri ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya USAID AFYA YANGU kupitia ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) uliofanyika  leo Mei 6,2022 jijini Dodoma.

Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akiyakaribisha mashirika na tasisi za kimataifa ambazo bado hazijapata ofisi katika mkoa huo kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupata ardhi ili wajenge ofisi wakati wa uzinduzi wa Mradi wa  USAID AFYA YANGU kupitia ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) uliofanyika leo Mei 6,2022 jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati akizindua  Mradi wa USAID AFYA YANGU leo Mei 6,2022 jijini Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua  Mradi wa USAID AFYA YANGU leo , Mei 6, 2022jijini Dodoma. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,  Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright ,  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula,Mwishi kulia ni Katibu Mkuu wa Afya Prof.Abel Makubi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha bango baada ya kuzindua  Mradi wa USAID AFYA YANGU kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 6, 2022.  Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,  Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright  na kulia ni  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka.

Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Afya Yangu Northern, Dr. Sajida Kimambo – amelishukuru shirika la USAID kwa ufadhili wa mradi huo utakaotekelezwa kanda ya kati na kaskazini na shirika la EGPAF na mashirika wenza ambao ni Amref, Matchboxology, D Tree, na Engenderhealth. Mradi huu utalengea kuwafikia watanzania moja kwa moja kwa kutoa huduma za VVU, Kifua Kikuu na Uzazi wa Mpango

………………………………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,amezindua Mradi wa USAID AFYA YANGU huku akisema kuwa  Serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele kuboresha huduma za afya ili kupambana na vifo vya Mama na Mtoto.

Waziri Mkuu ameyasema leo Mei 6,2022 jijini Dodoma wakati akizindua mradi wa AFYA YANGU inayotekelezwa hapa nchini kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa miaka mitano.

Amesema kuwa katika kutekeleza hilo serikali ilianza na kuboresha vituo vya afya ambapo hadi kufikia mwaka 2020 vituo 487 vya afya vilikuwa vimejengwa na hospitali za wilaya 102 zimejengwa na kukarabatiwa

Aidha Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na wadau wamefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha maambukizi ya virusi vya ukimwi yanapungua nchini ambapo jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda.

“Hadi kufikia Disemba mwaka jana asilimia 89 ya watu walikuwa wanatambua hali yao ya maambukizi huku asilimia 85.5 ya watu wanaoishi na maambukizi ya vurusi vya ukimwi walikuwa kwenye dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo hayo ni maendeleo makubwa yanatokana na utendaji wa serikali pamoja na wadau,”amesema 

Amesema kuwa mradi huo una nia ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma ya afya ya uzazi hapa nchini ambao unalenga kumuwezesha mtu binafsi aweze kuimarisha uwezo wake wa kuwa na tabia chanya katika kuzingatia mahitaji ya afya yake.

Malengo mengine ni kumuwezesha mtu kujihudumia mwenyewe pamoja na upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kwa mtu binafsi.  Pia, umelenga kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi na mtoto.

“Tunampongeza Rais Samia kwa dhamira yake ya kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi za vijiji na awapongeza USAID tawi la Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhimarisha huduma za afya kwa utekelezaji wa afua za kifua kikuu,ukimwi,uzazi wa mpango na maambukii ya ukimwi,”amesema

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali ya Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) imetoa ufadhili wa miradi mitatu ya USAID Afya Yangu kwa Mashirika ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Jhpiego, Deloitte kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa Comprehensive Client Centered Health Program (C3HP) unaotekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba 2021 hadi Oktoba 2027.

Hata hivyo  Waziri Ummy ametoa shukrani kwa  Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID Tanzania) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za afya nchini.

‘Shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali katika kutoa ufadhili wa utekelezaji wa afua za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango, pamoja na Afya ya Mama na Mtoto zitakazokuwa zinatekelezwa na miradi hiyo ya USAID Afya Yangu ambayo wanufaika wa mwisho kabisa ni Watanzania hasa wale walio maeneo ya pembezoni ya mikoa ambayo miradi hii itatekelezwa”amesema 

Naye Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Donald Wright, amesema urafiki na Ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani umeendelea kukua na kuimarika siku hadi siku jambo ambalo linachangia Ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Nchi ya hizo.

“Marekani imeendelea kuwa rafiki na mdau mkubwa wa maendeleo kwa Watanzania, uzinduzi wa mradi huu ni kithibitisho cha namna ambavyo tumejikita katika kuhakikisha tunashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya Watanzania katika Sekta za Afya, Miundombinu, na Uchumi.”

Awali, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri amesema kuwa USAID Afya Yangu ni programu ya miaka mitano, inayojumuisha miradi itakayoshughulikia masuala ya VVU, Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango, Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana.

Bi.Somvonsiri amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina takriban watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, inakabiliwa na changamoto za afya ya uzazi, watoto wachanga na vijana na inaendelea kuwa na kesi za UVIKO-19 ambazo zimeathiri makundi hatarishi kama vile akina mama wajawazito na watu wanaoishi na VVU.

“Serikali ya Marekani imedhamiria kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ngazi ya Serikali kuu na mikoa kutoa huduma bora za kinga, matunzo na matibabu ya VVU.

“Tunaipongeza serikali ya Tanzania na Wizara ya afya kwa ushirikiano tunaopata katika kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu afya za wananchi wake na katika mpango kazi huu wa miaka mitano tumejipanga na tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali itakayoleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla,”amesema

Kwa upande wake Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ametumia  fursa hiyo kuyakaribisha mashirika na tasisi za kimataifa ambazo bado hazijapata ofisi katika mkoa huo kufika ofisini kwake kwaajili ya kupata ardhi ili wajenge ofisi.

“Natumia fursa hii kuwakaribisha Dodoma makao makuu ya nchi na kwa mashirika ambayo hayajapata ofisi wafike ofisi tutawapa ardhi ili wajenge ofisi zao hapa yalipo makao makuu ya nchi na serikali,”amesema

About the author

mzalendoeditor