Featured Kitaifa

SHEHENA YA KWANZA YA PARACHICHI KUTOKA TANZANIA YAWASILI NCHINI INDIA

Written by mzalendoeditor

Balozi
wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega amepokea kwa
mara ya kwanza shehena ya matunda aina ya Parachichi kutoka Tanzania ikiwa ni
mwendelezo wa juhudi za Ubalozi huo za kutafuta masoko ya bidhaa za mazao ya
mbogamboga na matunda nchini India.

 

Akizungumza
na Naibu Mwenyekiti wa Bandari ya Jawalarlal Nehru ya mjini Mumbai, Bw. Unmesh
Sharad Wagh mara baada ya kupokea shehena hiyo iliyowsili tarehe 04 Mei 2022, Balozi Mbega ameishukuru
Serikali ya India kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye sekta
mbalimbali ikiwemo Kilimo na kwa pamoja na Bw. Wagh walikubaliana kushirikiana
katika sekta ya uchukuzi hususan katika kubadilishana ujuzi kwenye masuala ya
Bandari.

 

Katika
maelezo yake Balozi Mbega amesema kuwa, wafanyabiashara wa India wamehamasika kutokana
na juhudi za uhamasishaji zinazofanywa nchini humo na Ubalozi kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali wa hapa nchini na sasa wapo tayari kuanza kuingiza matunda
aina ya Nanasi na Embe kutoka Tanzania.

 

“Huu
ni mwendelezo wa juhudi za Ubalozi kwa kushirikiana na Serikali na TAHA wa
kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa za mazao ya mbogamboga na matunda nchini
India. Wafanyabiashara wa India wamehamasika na sasa wanakamilisha taratibu za
kuanza kuingiza nanasi na embe za Tanzania nchini India, amesema Balozi Mbega.  

 

Pia,
Balozi Mbega amekishukuru Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda Tanzania
(TAHA) kwa ushirikiano wao uliofanikisha shehena hiyo ya Parachihci kuwasili
India salama.

 

Shehena
hiyo ya kwanza ya parachichi  imewasili
nchini India kupitia Bandari yaJawalar Nehru ya mjini Mumbai kwa ushirikiano
kati ya Kampuni ya IG Fruits ya India na Kampuni ya Avoafrica ya Makambako
mkoani Iringa.

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega (kushoto mwenye miwani myeusi) akikata utepe wakati wa mapokezi rasmi ya Kontena lenye matunda aina ya Parachcihi kutoka Tanzania lililowasili nchini humo tarehe 04 Mei 2022 kupitia Bandari ya Jawalar Nehru ya mjini Mumbai. Kontena hilo la Parachichi limewasili nchini humo kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya IG Fruits ya India na Kampuni ya Avoafri ya Makambako mkoani Iringa. 
Balozi Anisa (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa bandari ya Mumbai baada ya kupokea na kufungua Kontena lenye Parachichi kutoka Tanzania
Picha ya pamoja
Balozi Anisa akiwa kwenye mazungumzo na Naibu Mwenyekiti wa Bandari ya Jawaharlal Nehru ya Mumbai, Bw. Unmesh Sharad Wagh baada ya kupokea matunda hayo ya parachichi  kutoka Tanzania. Katika mazungumzao yao walikubaliana kushirikiana katika kubadilishana ujuzi kati ya Tanzania na India kwenye masuala ya Bandari 


About the author

mzalendoeditor