Featured Kitaifa

RC MTAKA:‘WAGONJWA WA FISTULA ACHENI KUJIFICHA NDANI, NENDENI MKAPATE MATIBABU’

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akizungumza na wataalamu wa afya (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kambi ya utoaji wa matibabu ya fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wakina mama na Upasuaji wa Fistula na Rais wa Chama cha Madaktari wa Fistula Tanzania Dkt. James Chapa akizungumza na baadhi ya wataalamu wa afya wakati wa uziduzi wa kambi ya utoaji wa matibabu ya fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

BAADHI ya Wataalamu wa afya pamoja na Wananchi wakifatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa   uzinduzi wa kambi ya utoaji wa matibabu ya fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akizungumza na wataalamu wa afya (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kambi ya utoaji wa matibabu ya fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

………………………………………………..

Na Bolgas Odilo- Dodoma.

WANAWAKE wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Fistula Mkoa wa Dodoma wametakiwa kuacha kujificha ndani kwa kuona aibu badala yake waende kupata matibabu ambayo yanapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Hayo yamesemwa mapema leo Mei 3, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka wakati akizindua kambi ya utoaji wa matibabu ya fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Mtaka alipongeza hatua na jitihada zinazofanywa na wadau wa Fistula nchini na kuahidi kuwapa ushirikiano katika kutimiza dhamira yao ya kupunguza Festula nchini mpaka itakapofika mwaka 2030.

“Nitoe rai kwa wanawake wote wanaosumbuliwa na magonjwa ya fistula waache kujificha kwa kuona aibu badala yake waende kupatiwa matibabu kwakuwa huduma hiyo inapatikana hapa kwenye hospitali yetu ya rufaa mkoa wa Dodoma.

“Kuendelea kujificha kuendelea kujisababishia matatizo mengine makubwa zaidi, hivyo mjitokeze kupata matibabu,” alisema Mtaka.

Aidha aliwapongeza wadau wa Fistula nchini kwa kuendelea kutoa huduma hiyo kwa wananchi kwa kuwa ugonjwa huo ni moja kati ya magonjwa yenye changamoto nchini.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wadau wote wa Fistula kwasababu huu ugonjwa umekuwa ni kati ya magonjwa yenye changamoto hapa nchini  hivyo nawashukuru sana kwa hili na nitawaunga mkono,” alihitimisha Mtaka.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wakina mama na Upasuaji wa Fistula na Rais wa Chama cha Madaktari wa Fistula Tanzania Dkt. James Chapa aliahidi kushirikiana na madaktari bingwa wenzake ili kuhakikisha wanapunguza kiwango cha kuenea kwa ugonjwa wa Fistula nchini kufikia mwaka 2030.

About the author

mzalendoeditor