Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wenzake wa Afrika kujitahidi kushirikiana na vyombo vya habari na kukuza uhuru wao ili waweze kuchangia kikamilifu katika kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
Rais Samia ameongelea umuhimu wa nafasi za waandishi hao jijini Arusha katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani uliojumuisha waandishi mbalimbali barani Afrika.
Hata hivyo, Rais Samia amewasihi waandishi wa habari kuzungumzia pia mazuri ya bara la Afrika akisistiza walitetee, walisemee, walilinde bara lao na wasisite kujivunia na kutukuza kilicho chao.
Rais Samia amesema Bara la Afrika mara nyingi limekuwa likionekana kama lenye maovu tu hivyo ni wajibu wa waandishi kujenga taswira chanya, kwa mfano badala ya kuzungumzia migogoro na umaskini wazungumzie amani na maendeleo.
Pia Rais Samia amewasihi waandishi wa habari kuzitunza na kuheshimu mila na desturi za Kiafrika na kuzizungumzia kwa wingi na kuzitaka zile zilizo potofu zipigiwe kelele na jamii ielimishwe.
Wakati huo huo, Rais Samia amesema alielekeza kufanyike mchakatao wa marekebisho ya Sheria kwa njia ya majadiliano na kusikiliza matakwa ya waandishi wa habari ili tasnia ya habari ikae vizuri.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa mitandao ya kijamii ni sekta muhimu katika maisha yetu kwani hutumika kuunganisha jamii kwa maendeleo, kupeana pole panapotokea misiba, kupeana moyo katika mambo mbalimbali na pia kukubaliana na kutokukubaliana.