Featured Kitaifa

KUNDO ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI ANWANI ZA MAKAZI KATAVI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi, Kundo Mathew akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko (mwenye suti nyeusi) wakati akikagua utekelezaji Operesheni Anwani ya Makazi (kibao cha mtaa), leo mkoani Katavi.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi Kundo Mathew akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko (mwenye suti nyeusi) wakati akikagua utekelezaji Operesheni Anwani ya Makazi (namba ya nyumba), leo mkoani Katavi.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akionesha vibao vya ofisi mbalimbali wakati alipotembelea Karakana ya kutengeneza  nguzo na vibao vya Anwani ya Makazi, leo mkoani Katavi.

Picha na Jumaa Wange

…………………………………………………….

Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Katavi

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amefurahishwa na utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi mkoa wa Katavi ambapo katika kazi ya kukusanya taarifa mkoa huo umefikia asilimia 97.62.

Akizungumza leo, mkoani Katavi wakati alipokuwa katika ziara yake ya  kukagua  utekelezaji na uhamasishaji wa Anwani za Makazi, Naibu Waziri alisema kuwa mkoa  huo unastahili kupongezwa kutokana na utekelezaji wa Operesheni  Anwani za Makazi ilivyofanikiwa ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya fedha.

“Hadi Aprili 25, 2022 Mkoa wa Katavi umetekeleza kazi hii ya kukusanya taarifa kwa wastani wa asilimia 97.62 ambapo Halmashauri zote zimetekeleza kazi hii kwa zaidi ya asilimia 90 zikiongozwa Halmashauri za Wilaya ya Mpimbwe, Mlele na Tanganyika zilizotekeleza kwa zaidi ya asilimia 100. Nawapongeza sana kwa mafanikio haya, Halmashauri zilizosalia zikamilishe maeneo yaliyosalia ili zote zifikie malengo.” Alisema Naibu Waziri Kundo.

Alisisitiza “Nimeridhika na utekelezaji wa Anwani za Makazi katika mkoa huu, pia mmefanya vizuri kwa kuonesha mchanganuo wa mapato na matumizi ya fedha katika utekelezaji wa zoezi hili, pia ni vizuri kuhakikisha Wakaguzi wa Ndani kupitia halmashauri zetu wanaangalia matumizi ya fedha.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwamvua Mrindoko alisema kuwa licha ya mafanikio hayo ya mkoa wake katika utekelezaji wa zoezi hilo kumekuwepo na changamoto kadhaa ikiwemo mwitikio mdogo wa wananchi juu ya utengenezaji wa vibao na nguzo kwa ajili ya makazi na bararabara au mitaa na hivyo mkoa wake unaendelea kutatua changamoto hizo ili kufanikisha uwekaji wa Anwani za Makazi kwa wakati.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Kundo alisema kuwa Serikali inaweka mfumo wa Anwani za Makazi ikiwa ni   nyenzo ya kuwasaidia wananchi kujiletea maendeleo sambamba na kusaidia Taasisi mbalimbali katika kuhudumia Watanzania.

Aliongeza kuwa, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zilizoandika historia duniani kwa kuwa na mifumo ya Anwani za Makazi endapo mifumo hiyo itasimikwa vizuri nchini na kutimiza dhamira ya Serikali ya kufikisha huduma kwa wananchi kwa urahisi.

 “Tanzania inaandika historia ya kuwa na mifumo ambayo inaenda kufikisha huduma kwa wananchi tena kwa urahisi zaidi, lakini pia zoezi hili  la Anwani za Makazi litakapokamilika litasaidia kujua idadi ya watu katika eneo husika na Bunge litapanga mipango yake kulingana na mahitaji ya nchi yetu” Alisema Naibu Waziri Kundo.

About the author

mzalendoeditor