Featured Kitaifa

GST KUSOGEZA HUDUMA ZA MAABARA KWA WADAU,KUANZA NA GEITA

Written by mzalendoeditor


 
Na Mwandishi wetu-Dodoma

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu mwelekeo wake kwa siku za usoni kuwa ni pamoja  na kutumia ndege  isiyo na rubani kufanya tafiti za kina ili kuboresha shughuli hizo kwa lengo la kupata matokeo yenye tija zaidi.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba wakati akitoa mada kwa kamati  hiyo katika Semina iliyofanyika ukumbi wa AbdulKarim Mruma- GST , jijini Dodoma na kuhudhuriwa  na wajumbe wa kamati hiyo pamoja na viongozi waandamizi kutoka wizarani.

Ameongeza kuwa, kutokana na ukuaji wa tekinolojia duniani ikiwemo mahitaji ya sasa ya madini ya  viwandani na kulingana na utajiri wa rasilimali madini ambayo nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa nazo, mweleko wa GST ni kufanya tafiti kwa kutumia njia hiyo ili kuyafikia maeneo mengi na kwa haraka.

Aidha, Dkt. Budeba ametaja mwelekeo mwingine wa GST kuwa ni kufanya uchorongaji wa kimkakati ili kupata taarifa za uhakika za madini, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara ikiwemo Shirika la Madini  la  Taifa (STAMICO) pamoja na kuhakikisha inafungua Ofisi za GST kwenye Kanda ili kuigawa jiolojia kuwawezesha wachimbaji wadogo na wadau wengine kupata huduma katika kanda hizo kwa uharaka.

Pia, Dkt. Budeba amesema kuwa taasisi hiyo iko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya utoaji kitabu cha madini ya viwandani yanayopatikana nchini ambayo yanahitajika sana kwenye soko la dunia ambapo kitabu hicho kitawawezesha wadau kujua maeneo ya uwekezaji.

 Kwa niaba ya Meneja Ukaguzi wa madini na Uchunguzi, Mhandisi Priscus Kaspana ameieleza kamati kuwa,  GST imepanga kusogeza huduma za maabara kwa wateja  kwenye mikoa na kanda mbalimbali  na kwa kuanzia, itaanza na Mkoa wa Geita lengo likiwa ni kupanua wigo wa utoaji huduma za GST.

Akizungumzia historia ya uanzishwaji wa maabara ya GST, amesema ilianzishwa mwaka 1929 na imefahamika zaidi mwaka 2017 baada ya maboresho ya Sheria ya madini na baada ya kupata ithibati ya kuchunguza kilichopo kwenye sampuli kabla ya kupelekwa nje ya nchi.

Hivi karibuni wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya wizara kwa kamati hiyo kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2022, Dkt. Budeba aliieleza kuwa, taasisi hiyo imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kupata idhibati mbili  (2)  za njia  mbili za uchunguzi wa sampuli za madini na kuzitaja kuwa ni njia ya uchunguzi wa sampuli za dhahabu kwa njia ya Aqua Regia na upimaji wa kiwango cha majivu katika makaa ya mawe kwa njia ya gravimetric.

Naye, Mkurugenzi wa Kanzi Data wa  GST Terence Ngole  akiwasilisha mada kuhusu kurugenzi hiyo ambayo inayohusika na masuala ya ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za tafiti, amesema kuwa, GST ina utajiri wa taarifa nyingi za tafiti za madini ambazo zimekusanywa tangu kabla na baada ya kupatikana uhuru  wa Tanzania na kuongeza kuwa, taasisi hiyo imewahi kushinda kwa kuandaa chapisho bora  la masuala ya tafiti mwaka 2014.

Akifunga semina hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wa Kamati,  Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhandisi Stella Manyanya ameipongeza wizara kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa kamati hiyo ambao unaisaidia kutoa michango yenye afya ambayo inaiwezesha kuboresha utendaji wa wizara.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameihakikishia kamati hiyo kuwa, itaendelea kuufanyia kazi ushauri unaotolewa na kamati hiyo ikiwemo kujibu hoja zinazotolewa ambazo zinalenga kuboresha maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.

Awali, akizungumza katika mahojiano maalum, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula amesema kulingana na mahitaji ya dunia kwasasa madini ya kimkakati yanahitajika sana, akitolea mfano wa  miongo miwili ijayo, amesema mahitaji hayo yatapanda kwa asilimia 400 hadi 4000, hivyo kuitaka Serikali  kuitumia GST kufanya tafiti za kina kujua hali halisi ya uwepo wa madini hayo.

“ Kuiweka GST  kufanya utafiti wa awali tu kamwe hatutafika tunakotaka kwenda hivyo ni lazima tuwe na mawazo ya pamoja  kama kamati tuiwezeshe GST  kwa namna yoyote ili ifanye utafiti wa awali na wa kina,’’ amesema Kitandula.
Pia, ametaka taasisi hiyo kujengewa uwezo ili kuendana na  mabadiliko ya tekinolojia.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Budeba, GST ilianzishwa mnamo mwaka 1925 ikiwa  ni Idara chini ya utawala wa Mwingereza na ilikuwa taasisi mwaka 2017 baada ya kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Madini.

About the author

mzalendoeditor