Featured Kitaifa

WANANCHI MVOMERO WATAKIWA KUWA WAVUMILIVU WAKATI SERIKALI INATATUA MGOGORO WA MIPAKA YA HIFADHI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja  amewataka wananchi wa wilaya ya Mvomero hususan katika vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Wami-Mbiki kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa mipaka katika hifadhi ya Wami-mbiki.

Ameyasema hayo leo Aprili 20,2022 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Mhe. Jonas Van Zeeland, aliyetaka kujua lini Serikali itatatua mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Wami-mbiki na Wananchi wa Vijiji vinavyopakana na Hifadhi hiyo.

Aidha, amesema kuwa Serikali kupitia maamuzi ya Baraza la Mawaziri imeshaanza kuitatua migogoro hiyo.

“Utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri ulianza tarehe 05 Oktoba, 2021 kwa Mawaziri wa Kisekta na wataalam kupita katika Mikoa yenye migogoro ikiwemo mkoa wa Morogoro” Mhe. Masanja amesema.

Ameongeza kuwa wataalam kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na Wilaya husika wamepita katika vijiji vyote 24 vinavyopakana na Pori la Akiba Wami-Mbiki ambapo baadhi ya mipaka ya vijiji imeonekana kuwa na muingiliano na Mipaka ya Pori la Akiba Wami-Mbiki.

Pori la Akiba Wami-Mbiki linapakana na vijiji 24 ambapo vijiji nane (8) vipo upande wa Wilaya ya Mvomero na vijiji vitatu (3) vipo upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Aidha, vijiji 13 vipo upande wa Wilaya ya Chalinze – Mkoani Pwani

About the author

mzalendoeditor