Featured Kitaifa

TET KUWAPIGA MSASA WALIMU 120 WANAOFUNDISHA MASOMO YA UFUNDI

Written by mzalendoeditor

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), inaendesha mafunzo kazini kwa walimu 120 wa masomo ya ufundi katika shule za sekondari za serikali na zisizo za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Mafunzo hayo yanafanyika Mkoani Tanga katika shule ya ufundi Tanga (Tanga technical school) kuanzia tarehe 20/04/2022 na kutarajiwa kumalizika tarehe 25/04/2022.

Akifungua mafunzo hayo ya siku sita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bwana Ali Khamis amesema, mafunzo hayo yanalenga kuboresha utaalamu wa walimu na kuwezesha ujifunzaji wa masomo ya michepuo (Ufundi, Biashara, Kilimo na Maarifa ya nyumbani).

“Napenda niwakumbushe kupitia kwenu taifa linatarajia kupata wahitimu waliobobea na wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa katika fani mbalimbali ikiwemo ufundi mitambo, umeme, vifaa vya mawasiliano na ujenzi”.Amesema

Ameeleza pia kupitia mafunzo hayo Serikali inatarajia wanafunzi wakiandaliwa vizuri wataweza kujiajiri na kutengeneza ajira kwa watu wengine.

Amesema malengo hayo yakifikiwa, taifa litaweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuwa litakuwa na vijana wenye uwezo wa kutumia maarifa ya ufundi katika kufikiri, kubuni na kuunda vifaa na nyenzo za kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Ameeleza pia mafunzo hayo yamedhamiria katika kukuza stadi za karne ya 21 ambazo ni mawasiliano, ushirikiano, ubunifu na fikra tunduizi.

Pamoja na mambo mengine, alisema serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa za kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu ili kuboresha taaluma na utaalamu wao katika masomo mbalimbali yakiwemo masomo ya ufundi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema Serikali inatarajia kupitia mafunzo hayo walimu wataimarishwa katika ufundishaji wa masomo ya ufundi kwa kuzingatia ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia umahiri.

Ameeleza sababu kubwa ya kuanza na kundi hili la walimu wa michepuo ni kuwa Mihtasari ya masomo hayo iliboreshwa kati ya mwaka 2018 na 2019.

“Kwa kawaida tunapoboresha Mitaala au Mihtasari, huwa ni muhimu sana kuwapitisha walimu kwenye maboresho yanayofanyika ili kuwawezesha kutekeleza mtaala kwa mafanikio” amesema Dkt.Komba.

Aidha amesema ili mafunzo hayo waweze kuwafikia walimu wote, TET imelenga kushusha mafunzo hayo katika ngazi za chini/karibu na walimu kwa kuweka mazingira ya wawezeshaji wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini katika ngazi ya shule, klasta na vituo vya mafunzo ya walimu (TRCs)

Naye Mkurugenzi Msaidizi, Elimu ya Sekondari, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bi.Hadija Mcheka ameishukuru TET kwa kuendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu na amewataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo watakayopata kwa ufasaha.

¬†“Tunachopata tukakitumie ipasavyo tusiende kukaa nayo tu bali tukawape uzoefu wenzetu tuliowaacha shuleni kufanya kazi kwa ushirikiano na kuyasambaza kwa wanafunzi.” Amesema.¬†

Mwisho ameeleza kuwa Serikali inatarajia kuona ufaulu katika shule unaongezeka kupitia mafunzo hayo.

About the author

mzalendoeditor